January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Liliani Badi mwenyekiti mpya NaCoNGO

Na Zena Mohamed, Timesmajira Online,Dodoma.

BARAZA la Taifa la Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NaCoNGO) limepata viongozi wapya kama ambavyo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima alivyoagiza na kutoa siku 30, kwa Baraza hilo kufanya uchaguzi.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo,Mwenyekiti wa Kamati ya mpito iliyosimamia uchaguzi huo,Flaviana Charles amesema, Waziri Dkt. Gwajima alifanya uteuzi wa kamati ya mpito kwa ajili ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo iliundwa na wajumbe 10 kutoka Katika mashirika yasiyo ya kiserikali ya kitaifa.

Akitaja matokeo ya uchaguzi huo Flaviana amemtaja Liliani Badi kuibuka na ushindi mara baada ya kupata kura 21 huku Jane Magigita akipata kura 8.

Katika nafasi ya Katibu Mkuu,wajumbe hao wamemchagua, Revocatus Sono kwa kura 22 huku Gifti Kilasi akiambulia kura 7.

Nafasi ya Mwekahazina wajumbe hao wamemchagua John Kiteve kwa kura 15 huku Miraji Malinda akipata kura 13 na nafasi ya Kamati ya Fedha na Utawala wajumbe hao wamempigia kura za ndio Gaidon Haule ambaye alikuwa peke yake katika nafasi hiyo.

Katika kamati ya maadili wajumbe hao wamemchagua Novatus Marandu ambaye amepata kura 15 na Kamati ya Maendeleo na Uwezo akichaguliwa Rhobi Samweli,Kamati ya Utandaa na Mawasiliamo akichaguliwa Asifiwe Mallya huku wajumbe wanne wa Bodi wakiwa ni Jane Magigita,Revocatus Sono,Paulina Majogoro na Baltazari Komba.

Naye Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo Lilian Badi,akizungumza baada ya kuchaguliwa amehaidi kuyatekeleza yale ambayo aliyaahidi wakati akiomba kura.

“Mengi tumezungumza tumetoa ahadi nyingi kwa pamoja tutaenda kuyafanyia kazi yale tuliyoaahidi kikubwa naomba ushirikiano,”amesema.

Kwa upande wake,Katibu mpya wa Baraza hilo,Sono amewashukuru wote waliomwamini kwa kumpigia kura ambapo amedai kwamba mchakato huo haukuwa mdogo.

Huku Mwekahazina mpya Kiteve amesema watakuwa wasiri wa vikao kwa kutokutoa siri huku akidai kwamba watatoa ushauri sahihi kwa viongozi wa juu.

“Tutaendelea kumshauri Mwenyekiti pamoja na wengine tutakupa ushauri unaofaa (Mwenyekiti) sisi hatutoi siri na tutakuwa wasiri wa vikao,’’amesema.

Naye Mbunge wa Viti Maalum kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs), Neema Lugangira amewataka viongozi wapya kutokufanya kazi kwa kificho na badala yake wanatakiwa kuwa wawazi katika mambo yao pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuonekana.

Pamoja nakuwataka kuwa wawakilishi wa NGOs zote kubwa na ndogo bila ya kuweka matabaka huku akisisitiza uchaguzi umeisha sasa ni wakati wa kuchapa kazi.

“Uchaguzi umeisha sasa tuwe pamoja.Rai yangu kamati ya mpito iendelee kuwa walezi wa hawa viongozi wapya,”amesema.