December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhojiwa TAKUKURU leo. (Picha na Joyce Kaisiki).

Lijualikali ahojiwa TAKUKURU, awageukia wabunge CHADEMA

Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online,Dodoma

MBUNGE wa Kilombero, Peter Lijualikali amesema,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ina taarifa zote za matumizi ya fedha za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hivyo inachofanya kuwahoji wabunge na viongozi wengine ni kutaka kupata uhakika.

Lijualikali ambaye ameshaomba kuhamia CCM mara baada ya Bunge la 11 kuvunjwa ,ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi mara baada ya kutoka kuhojiwa na TAKUKURU.

Kufuatia hali hiyo amewaasa wahojiwa wote kueleza ukweli wa kile wanachokijua kwani hata wakidanganya haitasaidia kitu.

Lijualikali ambaye ameingia katika mahojiano saa 2:20 asubuhi na kutoka saa 5:5 asubuhi amesema,wahojiwa wasiwe na hofu kwani mahojiano ni ya kirafiki na hakuna kitu kipya zaidi ya wanachokijua.

“Nilipokea wito,kimsingi mahojiano yalikuwa ya kirafiki hakuna kitu kipya,naomba nitoe ombi kwa wenzangu wote wanaoendelea kuitwa kwa ajili ya kuhojiwa,waseme ukweli tu,kimsingi TAKUKURU wamejipanga na wana kila ‘information’ (taarifa) hakuna cha kuwadanganya ni kama vile wanakuja kuthibitisha ,hivyo ukija sema unachokijua kama unafikiri unaweza kudanganya huwezi kufanya hivyo maana hapa hatumsingizii mtu wala hatudanganyi umma.” amesema Lijualikali.