Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu (TAFF), Peter Sarungi amesema kuwa huenda mashindano yao yakaanza kutimua vumbi mwezi ujao.
Awali mashindano hayo walipanga yafanyike mwezi huu lakini kutokana na ongezeko la wagonjwa walioambukizwa virusi vya ugonjwa wa Corona wameamua kupeleka mbele mashindano hayo kwa mwezi mmoja.
Ligi hiyo itashirikisha timu nne lakini pia wakiwa na mpango mkakati wa kujiimarisha zaidi kwa kuongeza idadi ya timu pamoja na kupeleka Ligi hiyo katika Mikoa mbalimbali na kisha Tanzania nzima.
Sarungi ameliambia Majira kuwa, baada ya Serikali kusogeza mbele kuanza kwa shughuli za michezo na sisi tumeamuakusogeza mbele mashindano yetu kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Amesema, kwa kipindi hiki ambacho michezo imeendelea kusimama wao kama viongozi bado wanaendelea na shughuli mbalimbali ikiwemo kuimarisha mpango mkakati wa kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa watu wenye ulemavu.
Tanzania ilifanikiwa kufuzu kucheza mashindani hayo yaliyopangwa kufanyika kati ya Uingereza au Costa Rica mwaka 2022, licha ya kupoteza mchezo wa kumsaka mshindi wa tatu kwa kufungwa goli 2-1 na Liberia katika mashindano ya Afrika yaliyofanyika Angola, mwaka jana.
Baada ya kupoteza mchezo huo, Timu ya Taifa ya soka kwa watu wenye Ulemavu ‘Tembo Warriors’ ilimaliza ikiwa nafasi ya nne, mshindi wa tatu akiwa Liberia , Nigeria akishika nafasi ya pili huku wenyeji wa mashindano hayo, Angola wakitwaa ubingwa wa Afrika wa mashindano hayo.
Mbali na mafanikio hayo pia, mshambuliaji wa Tanzania, Khalfan Majani anayeshikilia rekodi ya ufungaji bora kwenye klabu katika Ligi ya ndani na mfungaji bora wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CACAAF), aliibuka kuwa mfungaji bora wa baada ya kufunga goli sita huku pia akiweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee kufunga hat-trick.
Sarungi amesema kuwa, pia watahakikisha mashindano hayo yanaendelea kufanyika kila mwaka baada ya mwaka jana kushingwa kufanyika kutokana na Tembo Warriors kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati pamoja na yale ya Afrika lakini pia kuwa na muundo mzuri utakaowarahisishia kazi zao.
Lakini pia Sarungi amewataka wachechezaji mbalimbali kuendelea kuchukua hatua katika kipindi hiki ambacho Serikali imesimamisha michezo kwa muda usiojulikana kwani Afya ni muhimu zaidi kuliko burudani hivyo kwa sasa ni muhimu kuvumilia kulinda Afya zao.
Hata hivyo Sarungi amesema kuwa, kwa sasa bado wanahangaika kusaka wadhamini ambao watawasaidia kufanya ligi yao kuwa na msisimko pamoja na kuleta hamasa ligi hiyo kuchezwa kwenye Mikoa mbalimbali.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025