December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Learn Basketball Skills With ZYBA’ kuhitimishwa Oktoba

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

PROGRAM maalum ya mafunzo ya muda mrefu ya mpira wa kikapu kwa vijana wenye umri wa miaka 15-25 ya ‘Learn Basketball Skills With ZYBA’ yatafikia tamati Oktoba 10, 2020.

Mafunzo hayo yaliyozinduliwa Agosti 8 yanakwenda kuhutimishwa huku yakiwa yamewanufaisha zaidi ya vijana 160 kutoka visiwani humo.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Aziz Salim ameuambia Mtandao wa TimesMajira kuwa, toka wameanza kutoa mafunzo hayo hadi sasa zaidi ya vijana 160 wamenufaika na mafunzo hayo na wanatarajia ongezeko la vijana katika wiki tatu zilizosalia kabla ya kufungwa.

Amesema, kupitia mafunzo yaliyokuwa yakifanyika mwishoni mwa wiki, wamepata zaidi ya vijana 50 ambao wameunganishwa na baadhi ya timu ili kupata mafunzo zaidi ya mchezo huo kutokana na kile walichokionesha.

“Baadhi ya vijana ambao tulikuwa tukiwapa mafunzo tumewanganisha na baadhi ya timu ambazo zinafanya mazoezi kila siku ili kupata ushindani na kukuza viwango vyao na tunaamini kupitia mafunzo hayo tutazalisha wachezaji bora zaidi ambao faida yake tutakuja kuiona siku za mbeleni,” amesema Mkurugenzi huyo.

Amesema, katika kufunga mafunzo hayo kutakuwa na tukio la aina yake hivyo wadau mbalimbali wanatakiwa kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia kile kilichozalishwa na programu hiyo.

“Ufungaji wa mafunzo haya utakuwa kwa mfumo wa tamasha hivyo nitumie fursa hii kuwaomba wadau mbali mbali kutusaidia kufanikisha jambo hili kupitia msaada wa vifaa ama fedha kwa lengo la kukamilisha shughuli hii, kwani msaada wako unakwenda kwa vijana wa Taifa hili lakini pia wenye mahitaji na ndoto kubwa ambazo wanatamani zifanikiwe,” amesema Aziz.