Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
Wazazi na walezi nchini wamekumbushwa kuzingatia suala la kulea Watoto katika ngazi ya familia ili wapate huduma za malezi bora na upendo wa dhati kutoka kwa baba na mama pamoja na ndugu wa karibu.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum,Mwanaidi Ali Khamis wakati wa hafla ya kukabidhi sare na vifaa vya shule kwa vituo Tisa vya makao ya kulelea Watoto yatima Dar es salaam vilivyotolewa na Taasisi ya LALJI FOUNDATION.
“Sio kila mtoto anayelelewa katika vituo vya kulelea Watoto yatima hana wazazi bali kuna sababu mbalimbali ambazo zinapelea Watoto kulelewa katika vituo lakini Watoto wakilelewa katika ngazi ya familia itasaidia kupunguza idadi ya Watoto wanaolelewa katika vituo hivi” amesema
Aidha ameipongeza na kuishukuru taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kumuunga mkono Mh. Rais Dkt. Samia kuboresha mazingira ya sekta ya elimu nchini huku akitoa wito kwa wadau wengine kujenga utamaduni wa kusaidia watu wenye uhitaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya LALJI FOUNDATION Imtiaz Lalji amesema lengo la taasisi hiyo ni kuendelea kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji na akibainisha kuwa msaada huo waliotoa kwa Watoto yatima utawawezesha kielimu .
“Tunaelewa kuwa upatikanaji wa elimu na rasilimali muhimu kama vifaa vya shule ni nyenzo muhimu sana katika kufungua fursa za Watoto kutimiza ndoto zao hivyo basi hiyo ndo sababu kubwa ambayo imetupelekea kusaidia Watoto hawa kupata vifaa wanavyohitaji kufikia malengo yao ya elimu” amesema
Aidha ameishukuru serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kuweka mazingira bora kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo taasisi ya LALJI FOUNDATION kufanya kazi za kijamii kwa utulivu na ushirikiano mkubwa kutoka serikalini.
Imtiaz amepongeza juhudi na kazi kubwa inayofanywa na wasimamizi wa vituo vya kulea Watoto yatima nchini kwa kujitolea muda na nguvu zao katika kulea Watoto hao.
Akizungumza kwa niaba ya walezi wa vituo tisa vya kulelea Watoto yatima ambavyo vimepatiwa msaada huo Mama Mutemwa kutoka kituo cha kulea Watoto cha Bibi na Babu ameishukuru taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kutoa msaada huo kwani utasaidia Watoto hao kuhudhuria masomo bila changamoto ya vifaa na itawasaidia kutimiza doto zao huku akitoa wito kwa wadau wengine kuendelea kupeleka misaada kwani uhitaji bado ni mkubwa.
Naye Katibu wa LALJI FOUNDATION,Fatema Lalji amesema jumla ya Watoto 400 kutoka makao 9 ya kulea Watoto yatima Dar es salaam wamepatiwa msaada huo na kubainisha kuwa taasisi hiyo inasaidia vituo vya Watoto yatima kila mwisho wa mwaka kwa kuwapa sare za shule , mabegi, viatu, soksi kupitia mradi huo endelevu ambao unatekelezwa kila mwaka .
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango