January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LALJI foundation yakabidhi madawati 100 kwa Shule Kisarawe

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Taasisi isiyo ya kiserikali ya LALJI FOUNDATION imetoa msaada wa madawati 100 kwa shule za msingi mbili Wilayani Kisarawe ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha mazingira ya sekta ya elimu nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madawati hayo kwa shule za msingi Msanga na Bembeza makamu Mwenyekiti taasisi ya LALJI FOUNDATION, Mohamed Damji amesema kuwa wametoa madawati hayo kwaajili ya kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania kuboresha miundombinu na mazingira ya elimu nchini.

Aidha, Damji amewataka wanafunzi wa shule hizo kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao ikiwemo kuwa viongozi bora na kufanya kazi katika fani mbalimbali hapa nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Zuberi Kizwezwe ameishukuru taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kutoa msaada huo na kutoa wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano kutoka taasisi hiyo kutoa misaada mbalimbali katika jamii.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti amesema Wilaya ya Kisarawe itaendelea kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo katika mambo mbalimbali huku akishukuru na kuipongeza taasisi ya LALJI FOUNDATION kwa kuendelea kusaidia jamii ya watu wenye uhitaji.