December 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KWA TAARIFA YAKO: Ajifungia kichwa ili kuacha kuvuta sigara

Na Mwandishi Wetu

WATU wengi wamejaribu kuacha kuvuta sigara, wako waliofanikiwa na ambao hawakufanikiwa.

Katika jitihada za kupambana na uraibu huo, jamaa mmoja aliamua kujivalisha chanja kichwani kwa lengo la kusihinda vita ya kuvuta sigara. Katika tukio hilo la ajabu, mkewe ndio anayekaa na ufunguo na humfungulia wakati wa kula tu.

Ibrahim Yucel akiwa na mtoto wake Ayse katika matembezi

Kwa mujibu wa jarida la lugha ya Kingereza la nchini Uturuki, Hurriyet Daily News, Ibrahim Yucel,(42) alichukua hatua hiyo ili kutimiza azma yake ya kuachana na uraibu wa kuvuta sigara.

Mkewe aitwaye Kawthar, wote wakazi wa Kutahya nchini Uturuki wako kwenye ndoa kwa miaka zaidi ya 16 amekuwa akimsumbua mumewe mara nyingi kuacha kuvuta sigara. Yucel amejaribu mbinu mbalimbali lakini hakufanikiwa na kujikuta akirudia tabia hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Yucel aliunda kichanja chenye waya za chuma, ili kuingiza kichwa chake na kufunga kwa kufuli mbili. Lengo hilo lilitokana na hatua mbaya aliyofikia ya kuvuta pakiti mbili za sigara kwa siku kwa zaidi ya miongo miwili.

Kawthar anasema hatua hiyo imepitiliza lakini kwa sababu mumewe ametia nia kutimiza lengo hilo, basi hana budi kumuunga mkono.

Yucel amekuwa akivuta sigara kwa zaidi ya miaka miaka 26, alimkabidhi funguo za kichanja hicho mkewe na mwanaye wa kike kila alipotaka kutoka nyumbani kila siku, ili asiweze kufungua pale anapopatwa na hamu ya kuvuta sigara.

Miezi michache baada ya kumpoteza baba yake kwa ugonjwa wa saratani ya mapafu, ambayo wataalamu wanasema imesababishwa na kuvuta sigara, Yucel aliona sio jambo zuri kuendelea kuvuta sigara katika maisha yake kwani anaiweka familia yake hatarini haswa baada ya kuona yaliyompata baba yake mzazi.

Yucel alivutiwa na wazo la kofia ngumu za kuendesha pikipiki (helmet) na kuamua kutengeneza kichanja cha waya za chuma ambao utamzuia kuwasha sigara hata akizidiwa na hamu.

Alipeleka wazo lake kwa mafundi chuma lakini walikataa kumtengenezea hivyo aliamua kufanya mwenyewe. Aliunganisha waya za kopa kwa kuziweka karibu karibu ili kuhakikusha sigara haiwezi kupenya na kisha kuongeza sehemu mbili za kubana kufuli.

Akamkabidhi ufunguo mmoja mkewe na mwingine bintiye, Ayse miaka 14, ili iwe ngumu kuvua chanja hicho kila atakapotoka nyumbani na kupatwa na hamu ya kuvuta sigara.

Japokuwa ilimlazimu kupambana na uraibu huo unaosababishwa na hamu kubwa ya kuvuta sigara, Yucel pia imamlazimu kupambana na aibu ya kuvaa chanja hicho anapokuwa hadharani ili aweze kuishinda vita hiyo.

Hata hivyo taarifa hiyo haikueleza Yucel alivaa chanja hicho kwa muda gani na kama alifanikiwa katika mapambano hayo.