Na Philemon Muhanuzi, TimesMajira Online
MBWANA Ally Samatta namfananisha na nyota inayowaka na kulipaisha jina la Tanzania popote linapotamkwa. Ni sawa sawa na linapotamkwa neno Tanzanite lenye kumaanisha madini ghali yenye kupatikana ndani ya nchi hii pekee.
Samatta ni mchezaji mwenye uthubutu, haogopi kujaribu pale ambapo vijana wenzake wa kitanzania wanaogopa kujaribu kucheza mpira.
Hajawahi kupungukiwa nidhamu wala moyo wa kupigana. Kuhama kwake kutoka Aston Villa kwenda Fenerbahce ya Uturuki kumezua mpasuko wa mawazo miongoni mwa watu.
Wapo wenye kuamini kuwa Aston Villa haikuwa katika ngazi sawa ya kiwango cha ubora kwa kuilinganisha na Genk ya Ubelgiji aliyoichezea kabla ya kwenda Uingereza.
Wapo waliomtazama Samatta na kumuona kuwa ni mshambuliaji mwenye kupungukiwa nguvu kwa kumlinganisha na washambuliaji wengine wanaocheza namba tisa ambao ni waafrika wenzake wanaochezea timu za Uingereza. Lakini yote kwa yote ya Samatta ni safari chanya sana ya mchezaji mtafutaji wa maisha.
Naamini ndani kabisa ya nafsi ya Samatta angependa achezee timu kama Manchester United, Leicester City au Chelsea. Lakini ukipangacho sicho kile kinachopangwa na Mungu. Ni Aston Villa waliokuwa na nafasi kwa ajili yake.
Tena wakamchukua ili asaidie katika mapambano ya kuiokoa timu isishuke daraja, akaenda pale kama mwokozi badala ya kuwa mchezaji anayepambana ili timu imalize msimu ikishika nafasi moja kati ya zile nne za juu.
Muda mwingi akawa analazimika kushuka mpaka pale katikati ya uwanja, kwani timu nzima inakuwa ikishambuliwa na kulazimika kutumia mikakati ya ushirikiano wa kitimu (collective football).
Samatta wa Genk ni yule aliyekuwa akichezea timu yenye kushambulia muda mwingi, hakuwa sehemu ya kujihami ili timu ijiokoe isishuke daraja.
Ni kweli pia nguvu za mwili ni silaha ya mchezaji yoyote anayechezea ligi ya Uingereza. Mara nyingi akawa akisukumwa kidogo tu anaonyesha kutolewa njiani kirahisi.
Na magoli mawili tu aliyofunga katika mechi zote alizocheza kwa kweli hayafanani na malengo ya makocha waliomuona kule Ubelgiji na kuamini kuwa atakwenda kuwaokoa wasishuke daraja.
Hawakushuka kwa kuweza kupata pointi kadhaa zilizowabakiza ligi kuu lakini Samatta akaonekana kutolingana na ukubwa wa jina alilotoka nalo Ubelgiji.
Safari imeendelea Uturuki, klabu kongwe ya Fenerbahce imemnunua kwa kiwango cha paundi milioni sita. Hii klabu ni kubwa kulinganisha na Aston Villa ya sasa.
Hategemewi kuonekana muda mwingi akiwa maeneo ya katikati ya uwanja akijiandaa kusaidia kuzuia, anategemewa kuchezeshwa ili afanye kazi ya kufunga magoli.
Heshima ameshaitengeneza tayari. Mtanzania wa kwanza kuchezea timu ya ligi kuu ya Uingereza. Mchezaji wa pili kutoka ukanda wa Afrika ya mashariki.
Tena katika miaka hii ambayo vijana wengi wanakwenda huko nje na mwisho wa siku wanarudi nchini kutaka kuchezea Yanga na Simba.
Upambanaji wake hauwezi kuchekwa na mtu makini mwenye kufuatilia viwango vya wanasoka wetu vijana. Presha ya Fenerbahce haiwezi kuwa sawa na ile ya Aston Villa.
Na Uturuki hakuna ugumu kama ule wa Uingereza ambapo ni rahisi sana kwa wachezaji wa mbele kuumizwa kila wanapopamiwa na mabeki.
Na wafuatiliaji wa ligi kuu ya Uturuki hawana wingi kama wale wanaobeti kila zinapokaribia mechi za Uingereza.
Mfungaji akikosa goli katika mechi moja ya Uturuki hilo kosa haliwi ni maarufu kama akikosa mfungaji wa Manchester United dhidi ya Manchester City.
Hivyo mashabiki waliokuwa wakim-follow Samatta kule Uingereza wala hawana sababu ya kutukanana na wenye timu yao. Wajitoe tu na kuanza kumfuatilia katika timu yake mpya.
Ndio lulu yetu ndio kioo cha soka la Tanzania. Kijana wa miaka 27 akielekea 28 bado amejaa nguvu ya kufunga magoli muhimu huko Uturuki na pengine akanunuliwa tena na timu bora zaidi ya Uingereza kulinganisha na hii Aston Villa.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
Miaka 63 ya Uhuru na rekodi treni ya SGR