Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
ENEO la Kurasini Logistics Park linaloandaliwa kuwa Port Extension ya Bandari ya Dar es Salaam linatarajiwa kuanza kutumika rasmi mwezi Novemba mwaka huu, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa makontena na malori katika bandari hiyo.
Akizungumza Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa wakati wa ziara yake katika Bandari ya Dar es Salaam leo Agosti 21, 2026, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema eneo hilo limefikia asilimia 98 ya utekelezaji katika hatua ya awali, huku Serikali ikisisitiza litumike kama sehemu ya bandari badala ya kuwa Kituo Kikavu cha Mizigo (ICD).
Amesema matumizi ya eneo hilo kama Port Extension yatawezesha makontena yatakayoshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam kuhamishiwa huko kwa ajili ya taratibu za ukaguzi, clearance na hatua nyingine za kisheria kabla ya kukabidhiwa kwa wahusika.
Kwa mujibu wa Waziri Mbarawa, ili eneo hilo liweze kufanya kazi kikamilifu kama Port Extension, Serikali imeweka mambo mawili ya msingi, likiwamo kuhakikisha kuna mashine za kukagua mizigo (scanners).

Amesema mobile scanners zinaweza kuletwa katika eneo hilo ili kukagua makontena yote yatakayohamishiwa Kurasini, hatua itakayosaidia kupunguza mzigo wa shughuli katika eneo kuu la bandari.
Jambo jingine, amesema, ni kuhakikisha barabara inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kurasini Logistics Park inatambuliwa kama Customs Bonded Road, ambayo itaidhinishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwekwa mifumo ya ulinzi na ufuatiliaji ikiwamo kamera.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa sababu mizigo itakayotoka bandarini itaelekezwa moja kwa moja katika eneo la Port Extension ambako ukaguzi na taratibu nyingine za forodha zitafanyika.

Waziri Mbarawa amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekubaliana kukaa pamoja na kampuni ya Tangold, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Halmashauri husika, kuhakikisha barabara hiyo inakuwa maalumu kwa usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda Kurasini Logistics Park.
Amesema kwa kuanzia, eneo hilo litatumika zaidi kwa ajili ya makontena ya mizigo inayoingia nchini (import containers), huku mpango wa kushughulikia makontena ya mizigo inayotoka nchini (export containers) ukitarajiwa kufanyiwa kazi baadaye.

Aidha, amesema taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwamo TPA na TRA, zitakuwepo katika eneo hilo ili kuwezesha taratibu za ukaguzi, clearance na uondoshaji wa mizigo kufanyika huko badala ya wafanyabiashara kusubiri huduma zote katika Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema utekelezaji huo utakapokamilika utasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa makontena na malori katika Bandari ya Dar es Salaam, huku ukiongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa mizigo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus , amesema uwepo wa Kurasini Logistics Park ni muhimu katika kukabiliana na changamoto ya msongamano wa malori na mizigo inayotokana na kuongezeka kwa shughuli za Bandari ya Dar es Salaam.

Amesema kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikisogelewa zaidi na maeneo ya makazi pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii, hali inayosababisha kuongezeka kwa mwingiliano kati ya shughuli za kibandari na shughuli za watu binafsi wanaotumia miundombinu inayozunguka bandari.
“Ongezeko kubwa la shughuli za bandari limeongeza pia kiasi cha mizigo kinachopita katika eneo hilo, jambo ambalo limekuwa na athari katika miundombinu ya barabara kutokana na kuongezeka kwa idadi ya malori yanayoingia na kutoka bandarini,” amesema Abed.
Kwa mujibu wa Abed, katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025/2026, kiwango cha mizigo kinachohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kimeongezeka kwa takribani tani milioni sita, hali iliyoongeza mahitaji ya miundombinu bora ya kuhifadhi malori na mizigo.
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuwekeza katika miundombinu kama Kurasini Logistics Park, ambayo itakuwa na uwezo wa kuhifadhi malori pamoja na mizigo kabla ya kuondolewa katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Kurasini Logistics Park ni muhimu kwa sababu itasaidia kuhifadhi malori na mizigo kabla haijaondoka katika Bandari ya Dar es Salaam, hivyo kupunguza msongamano unaojitokeza katika maeneo ya bandari na barabara zinazozunguka,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuhakikisha ongezeko la mizigo haliathiri kwa kiwango kikubwa usafirishaji pamoja na matumizi ya miundombinu ya barabara.
Abed amemshukuru Waziri wa Uchukuzi kwa kutembelea eneo hilo na kutoa maelekezo kuhusu namna bora ya kutumia Kurasini Logistics Park, akiahidi kuwa uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam utatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa.
Amesema utekelezaji wa hatua hizo utasaidia kuboresha huduma za bandari, kupunguza msongamano wa malori katika maeneo ya jiji na kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

More Stories
Kairuki: TTCL ongezeni kasi ya Fiber majumbani
Makame awakalia kooni Ma-DC,utitiri vituo vya ukaguzi
Ujuzi wa Wezesha Binti wawasaidia vijana kujiajiri na kupata ajira