Na Zena Mohamed, Timesmajiraonline,Dodoma.
MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umesema kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri kujisajili na Mfuko katika kipindi cha awamu ya sita kutokana na hatua za makusudi za Serikali kuweka vivutio vya kufanya biashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya uchangiaji na msamaha wa riba.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 2,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Dkt.John Mduma wakazi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo.
Amesema kuwa hadi kufikia Juni 30 , 2022, mfuko huo ulikuwa umesajili jumla ya waajiri 27,786 ikiwa ni asilimia 90 ya waajiri 30,846 walioko kwenye kanzidata ya Mfuko.
“Waajiri waliosajiliwa wamegawanyika katika makundi matatu, kundi la kwanza ni la waajiri wakubwa ambao wanachangia kiasi kinachozidi Shilingi Milioni 1.5 kwa mwezi, kundi la pili ni la waajiri wa kati wanaochangia kati ya Shilingi 250,000 na Shilingi Milioni 1.5 kwa mwezi na kundi la tatu ni la waajiri wanaochangia chini ya Shilingi 250,000 kwa mwezi,”amesema Dkt.Mduma
Ambapo amefafanu katika makundi hayo WCF imesajili waajiri wakubwa asilimia 99.27 ya waajiri hao, waajiri wa kati ni asilimia 98.71 ya waajiri hao na waajiri wa chini ni asilimia 88.56 ya waajiri hao.
Aidha Dkt.Mduma amezungumzia makusanyo kutoka kwa waajiri ambapo amesema Mfuko huo ulianza rasmi kukusanya michango kwa waajiri kuanzia Julai Mosi 2015 na hadi kufikia 30 Juni 2022, makusanyo ya jumla ya michango yalifikia Shilingi Bilioni 545.49.
“Hadi kufikia 30 Juni 2022, Mfuko ulikuwa umekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 241.48 toka kwenye mapato yatokanayo na uwekezaji ambapo WCF ilitengeneza Shilingi Bilioni 69.86 katika mwaka wa fedha 2020/2021; na Shilingi Bilioni 74.29 katika mwaka wa fedha 2021/2022,”amesema.
Akizungumzia ulipaji wa fidia kwa wafanyakazi walioumia,kuugua ama kufariki kazini Dkt.Mduma amesema, kabla ya kuanzishwa kwa WCF, malipo ya fidia nchini kwa mwaka mzima yalikuwa chini ya shilingi milioni 200 lakini baada ya kuanzishwa kwa WCF malipo yanaongezeka mwaka hadi mwaka.
“Kwa takwimu za 2016/17,WCF ililipa fidia kwa wanaufaika takribani 538 na kiasi cha shilingi milioni 613.84 kililipwa, na kwa mwaka 2021/2022 pekee, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 1,600 na kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 9.33 kililipwa na hadi kufikia 30 Juni 2022, WCF imelipa mafao yenye thamani ya Shilingi Bilioni 44.61 kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko kubwa kwa kulinganisha na kipindi cha kabla ya kuanza kwa WCF,
“Kwa hesabu zisizokaguliwa,katika kipindi cha Julai 2022 hadi Desemba 2022,WCF ililipa mafao ya jumla yashilingi bilioni 6.19 kwa wanufaika 1,004 na hivyo kufanya wanufaika wa Mfuko toka kuanzishwa kwake kufikia 10,454 ambao wamelipwa jumla ya shilingi bilioni 49.44,”amesema.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa