Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
NAIBU Waziri wa Maji,Mhandisi Kundo Mathew,amewataka wananchi wa Wilaya ya Ilemela na Jiji la Mwanza kuwa walinzi wa dira za maji(mita za maji), ili kuepusha hasara kwa serikali kwani zinagharama kubwa.
Kundo amekerwa na vitendo vya wizi wa dira za maji unaofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu katika nyumba za watu waliounganishiwa huduma ya maji na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),huku akiwahimiza wananchi kulipa ankra( bili) za maji na kuepuka kutumia mbinu zisizo halali ambazo zinasababisha malalamiko ya kubambikiwa deni.
Hayo amebainisha wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu katika mkutano wa hadhara Julai 26,2024 uliolenga kusikiliza na kutatua changamoto na kero ya maji inayowakabili wakazi wa maeneo hayo.
“Mita ni mali ya mamlaka na zina gharama, imewekwa kwako unakuta haipo,sasa najiuliza,sisi tufanye je?,tusaidieni kuwa walinzi wa mita zenu wenyewe, kazi yetu kuhakikisha maji tunakusogezea karibu,msiharibu miundombinu ya maji wewe hata kama una hasira za namna gani usiende kumaliza hasira zako kwenye mabomba,”amesema Mhandisi Kundo.
Pia amewataka wananchi kudhibiti matumizi ya maji kulingana na kipato chao ili waweze kulipa bili za maji na wasikwepe kwa kutafuta njia mbadala ya kupunguza gharama za ulipaji huduma ya maji ambayo siyo halali.
Ambapo ametaja mbinu mbalimbali ambazo baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia kukwepa kulipa bili halali ya maji ikiwemo kumpa kiasi kidogo Msoma mita jambo ambalo ameeleza kuwa halimalizi tatizo na badala yake linafanya deni kuwa kubwa na kuibua malalamiko ya kubambikiwa bili.
“Msidanganyike kuna watu wengine msoma mita anakuambia nipe tu 20000 nakusomea mita bei ndogo wala hauta someka kwenye mfumo,hapo unahairisha deni tu na litakuwa palepale,Msoma mita yule akiondoka akaja mwingine deni lako kwenye kompyuta alijafutika kwa sababu hana mamlaka ya kufuata deni hilo, utaletewa bili ya 400,000 hadi 500,000, unaanza kulalamika kuwa umebambikiwa kumbe ulishirikiana na mtu wetu mmoja ambaye siyo muaminifu ukaona kwamba umewini sana mwenzio kaweka fedha mfukoni hakuna haki bila wajibu,”ameeleza Mhandisi Kundo na kuongeza kuwa;
“Sababu nyingine ni kuwa wanachukua betri ya saa unaenda kuweka kwenye mita alafu unaanza kupitisha maji ile mita itasimama haitosoma hautakuwa mjanja sana kwani kitendo hicho ni kuhairisha tatizo,baada ya muda fulani kumbukumbu ya mita inarejea na kusoma idadi ya maji yaliopita maana yake tutakupiga tena,sasa michezo yote hiyo tusiifanye,”.
Aidha ameeleza kuwa wengine wanabadili uelekeo wa mita na kusoma hasi(negative) ili bili halisi isitoke hivyo akija mkaguzi na akagundua kuwa ilibadilishwa atairudisha kawaida itasoma kila kitu kuanzia pale ilipogeuzwa hivyo amewataka kuacha na mambo hayo kwani hayana tija.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa uhaba wa maji jijini Mwanza,chanzo hakitoshelezi hivyo mradi wa Igombe-Kabangaja,ukikamilika utatoa maji ya uhakika na kuondoa changamoto hiyo kwa wakazi wa Ilemela.
“Uhaba wa maji pia unasababishwa na ongezeko la idadi ya watu na makazi mapya,ambalo linahitaji tupanue mtandao wa maji unaohitaji fedha changamoto haziwezi kwisha kwa wakati mmoja,”.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (NWAUWASA),Neli Msuya amesema mradi wa Matokeo ya Haraka unaogharimu bilioni 4.7 umechelewa kukamilika sababu ya ukosefu wa fedha.
“Mlioni 500 zilitolewa kuboresha mfumo wa maji Buswelu, hazikukidhi kufikisha maji maeneo yote kutokana na ukubwa wa tatizo hivyo tulibuni mradi huo wenye thamani ya bilioni 4.7 ambapo tumepokea bilioni 1.7 tukalaza mabomba umbali wa kilometa 14,”ameeleza Neli.
Naye Mbunge wa Ilemela Dkt.Angeline Mabula juhudi za kumtua mama ndoo kichwani zimeanza kuonekana,Ilemela imepata mradi wa maji wa Igombe-Kabangaja wenye thamani ya milioni 800 ukikamilika pamoja na chanzo cha Butimba, maji yatatosheleza.
Amesema mradi wa Matokeo ya Haraka, umekuwa na tija kwa kupunguza kero ya maji,changamoto ni vifaa anaamini itatatuliwa amemuomba Mkurugenzi wa MWAUWASA mifumo ikifunguka fedha zikaanza kutoka aje h Buswelu kuondoa tatizo la maji.
More Stories
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa