Na Penina Malundo,Timesmajira
Afya ya uzazi ni haki ya msingi ya binadamu inayohusisha ustawi wa kimwili, kiakili na kijamii wa mtu katika masuala yanayohusiana na mfumo wa uzazi.
Huku ikihusisha uwezo wa mtu kufanya maamuzi ya uhuru kuhusu uzazi, kupata huduma salama za uzazi wa mpango, kujifungua salama, na kupokea elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi.
Tanzania,kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono mikataba na maazimio mbalimbali yanayolenga kulinda na kuboresha afya ya uzazi kwa wanawake, vijana, na watoto lakini bado haina sheria maalum ya afya ya uzazi.
Ni ukweli usiopingika kuwa Afya ya uzazi imetambuliwa kimataifa kama sehemu ya haki za binadamu na inamaana kuwa kila mwanamke, mwanaume, na kijana ana haki ya kupata taarifa, elimu na huduma bora za uzazi bila ubaguzi.
Haki hizi zinajumuisha haki ya kufanya maamuzi kuhusu idadi ya watoto, muda wa kupata watoto, na haki ya kupata huduma za matibabu wakati wa ujauzito, kujifungua, na baada ya kujifungua.
Wakili na Mtaalamu wa Masuala ya Haki ya Afya ya Uzazi,Wakili Walta Carlos anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo inalenga kila nchi wanachama mikataba hiyo inahakikisha inatekeleza masuala ya afya ya uzazi kwenye nchi zao.
Anasema miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na Mikataba ya Kimataifa Tanzania iliyosaini na kuridhia kama Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Mtoto (CRC, 1989)ambapo Tanzania imejitolea kulinda afya ya watoto, ikiwemo wasichana wa rika balehe.
Mkataba unasisitiza wajibu wa serikali kutoa elimu ya afya ya uzazi, kulinda watoto dhidi ya ndoa za utotoni, mimba za mapema na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Pia anataja Mikataba ya Kikanda Tanzania iliyohusishwa Mkataba wa Maputo (Maputo Protocol, 2003)ambao ni mkataba wa Umoja wa Afrika unaolenga kulinda haki za wanawake, ikiwemo afya ya uzazi.
Anasema Tanzania iliridhia Mkataba wa Maputo mwaka 2007, na kupitia kipengele cha 14,mkataba unazungumzia haki ya wanawake kupata huduma za afya ya uzazi bila ubaguzi, upatikanaji wa huduma za mimba salama, na kulinda wanawake dhidi ya vitendo hatarishi kama ukeketaji.
”Pamoja na mikataba yote tuliosaini na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuainisha vifungu mbalimbali vya haki ya uzazi lakini bado tunachangamoto ya kutokuwa na sheria inayozungumzia masuala hayo ya afya ya uzazi,”anasema.
Anasema katika Mkataba wa Maputo Protocal ambao Tanzania ni miongoni mwa nchi 49 zilizosaini mkataba huo na kama nchi iliahidi kuja kuutumia nchini kama kuhakikisha haki za uzazi zinalindwa kwa wanawake,ikiwemo haki ya kupata huduma za uzazi wa mpango,haki za kuweza kujilinda na magonjwa ya zinaa na magonjwa ya kuambukizwa na kupinga ndoa za utotoni na mimba za utotoni na suala la Ukeketaji.
Carlos anasema sambamba na hiyo Tanzania bado inachangamoto kidogo ikiwemo kutokuwa na sheria maalum ya afya ya uzazi Tanzania.
”Tanzania Tumepokea Mkataba wa Maputo Protocal 2003 pasipo kuweka shaka yoyote na mkataba huu ni miongoni mwa mkataba unaolinda haki za afya ya uzazi.
”Hiyo ni changamoto kubwa na kama Maputo Protocal itafanywa kuwa miongoni mwa sheria za ndani ya nchi basi kutakuwa tumepata mabadiliko ya sheria ambayo yatakuwa yanalinda haki za Binadamu,”anasema.
Anasema anasema kama nchi inahitaji kutengeneza sheria za afya ya uzazi lakini pia kulinda masuala ya afya ya uzazi kwani ni kitu muhimu sana katika nchi na endapo haitawekwa sawa inaweza kuleta athari nyingi ikiwemo vifo kwa wanawake vitokanavyo na uzazi.
Kwa Upande wake Mkuu wa Ubora na Uboreshaji wa Sekta ya Afya na Umma kutoka Hospitali ya Maria Stopers,Dkt.Selemani Mbyallu kutoka Hospitali ya Maria stopers, anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imeingia mikataba mbalimbali katika kuhakikisha afya ya uzazi wa mpango inasimamia na kuwafikia wananchi mbalimbali.
“Tanzania hadi inapongia katika makubaliano ya kimataifa uwa inamaanisha kitu wanachokifanya kama ukiangalia makubaliano ya Maputo Protocal,ilivyohakikisha inasimamia ipasavyo makubaliano yao mbalimbali waliyojiwekea kama nchi mwanachama katika vipengele vya kuhakikisha Tanzania inasimama na masuala ya afya ya uzazi wa mpango na kuhakikisha watanzania wanapanga uzazi,”anasema
Anasema kuna vipengele ambavyo tayari wameanza kuvifanyia kazi katika makubaliano mbalimbali kama uhakikishaji wa utoaji wa huduma ya afya ya uzazi wa mpango bure katika vituo vyao vya serikali na kuhakikisha watoa huduma kupatiwa mafunzo maalum ambayo yataweza kuwasaidia katika utoaji wa elimu kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo,”anasema
Anasema ni kweli kuna baadhi ya vipengele ambavyo hadi sasa bado hawajaweza kukabiliana navyo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ambayo mifumo ya Tanzania bado inashindwa kuchukua hatua madhubutu kutokana na changamoto mbalimbali.
” Tanzania ni miongoni mwa mwanachama wa makubaliano mbalimbali ikiwemo Maputo Protocol ambapo kuna vipengele vingi ambavyo vipo na tumeanza kuvitekeleza ipasavyo na pia kunavipengele vingine ni vingumu kuvicopi na kunavipengele vingine mifumo yetu bado haijaanza kuruhusu na kushindwa kuvichukua,”anasema
Anasema kuna baadhi ya vitu vinakuwa vigumu kutokana na asili ya nchi,mila na desturi katika maisha yanayowazunguka watu lakini pia ipo vipengele vingine ambavyo bado Tanzania haijawafikia ambapo Tanzania inapambana katika kuhakikisha afya ya uzazi.

More Stories
Wanawake wa milimani waendelea kuumia licha ya ahadi za COP29
Taasisi nyingi,Serikali moja na misitu ya Kilimanjaro inayopotea
Ukusanyaji wa Taarifa na Hatari za Kutoa Taarifa Binafsi Mtandaoni