November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Kumtambua mzee hakuhitaji barua ya Mwenyekiti’

Na Omary Mngindo,TimesMajira Online. Mlandizi

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, Michael Mwakamo amesema moja ya jambo linalomkera ni kitendo cha watumishi sekta ya afya, kuwataka wazee wathibitishe uzee wao kupitia barua ya Mwenyekiti.

Hali hiyo inayolalamikiwa na wazee wengi kwenye zahanati na vituo vya afya maeneo mbalimbali, imekuwa kero kubwa ambapo mara kadhaa walengwa hao wanapokwenda maeneo hayo hutakiwa kuthibitisha umri kupitia barua.

Mwakamo ametoa kauli hiyo katika Kitongoji cha Vikuruti akiwa katika kampeni ya kukiombea kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wagombea wake Dkt. John Magufuli, Ubunge na Udiwani, Uephrasia Kadala na wagombea wote wa chama hicho.

“Jambo hili linanisikitisha sana na hii ni tabia ya baadhi ya watumishi ambao kwa matakwa yao ya maksudi wanapowataka wazee wetu waoneshe barua za uthibitisho wa uzee wao kutoka kwa Wenyeviti wa Vijiji au Vitongoji, ili nitakwenda kulifanyia kazi,” amesema Mwakamo.

Ameongeza kuwa kitambulisho cha kwanza kwa mzee ni sura yake, ambayo inajionesha wazi na kamwe haiwezi kulinganishwa na kijana, hivyo kitendo cha watumishi kudai barua ya Wenyeviti ni kuwasababishia usumbufu wazee, huku akiwataka waondokane na tabia hiyo.