September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kumbilamoto ‘abomoa’ matawi ya CUF Vingunguti

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

MGOMBEA wa udiwani wa Kata ya Vingunguti kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Omary Kumbilamoto amendelea kumwaga sera kwa wananchi na kuwaomba kura huku wanachama wa CUF wakihamia chama hicho kutoka Kata ya Vingunguti Manispaa ya Ilala.

Akipokea wanachama wapya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Ubaya Chuma amesema, hayo ni mafanikio mazuri ndani ya CCM kuendea kuzoa wanachama wa upinzani sera za CCM zinakubalika, wagombea wanakubalika na CCM itashinda kwa kishindo.

Akizungumza mambo aliyofanya katika Kata ya Vingunguti Omary Kumbilamoto amesema, katika uongozi wake wa miaka mitano iliyopita ameboresha huduma za afya ndani ya kata hiyo kwa kununua vifaa vya kisasa katika Zahanati ya Vingunguti pamoja na kuwakabidhi gari la wagonjwa ambayo inatumika mpaka sasa.

Omary Kumbilamoto amesema, mambo mengine ambayo amefanya katika kata hiyo kuboresha Ofisi za CCM za kata na matawi kwa sasa zinavutia.

Amewataka wananchi wa Kata hiyo wamchague mgombea Urais John Magufuli wampigie kura kwa kishindo pamoja na Mbunge Bonah Ladslaus Kamoli ili waweze kuwaletea maendeleo .

“Nawaomba wananchi wenzangu wa Vingunguti kura yangu ya Udiwani ,kura ya Rais John Magufuli na Mbunge wangu Bonah Ladslaus Kamoli ili tuweze kuibadilisha Kata hii iwe ya kisasa zaidi Serikali ya awamu ya tano imewaletea Machinjio ya Kisasa ni juhudi za Rais wetu John Magufuli na Bonah Kamoli katika kujenga Tanzania ya uchumi wa viwanda, ” alisema Kumbilamoto.

Amesema, mikakati yake mingine ndani ya kata Vingunguti akichaguliwa atawajengea barabara za kisasa katika mradi wa Serikali DMDP kwa ajili ya kuboresha miundombinu, kutoa ajira 300 kwa wakazi wa Vingunguti na kata za jirani mara baada machinjio hayo ya kisasa kukamilika.

Mikakati mingine kuwajengea soko la nyama taratibu zimeshafanyika nyumba 20 zitabomolewa kwa ajili ya mpango huo kuanza dhumuni kuongeza ajira kwa wananchi wa Vingunguti Manispaa ya Ilala.

“Siku ya Oktoba 28 ni siku ya mapumziko tujitokezeni tukapige kura wananchi wote wa Kata hii ya Vingunguti na mkinichagua kwa awamu ya pili kuwa diwani wa kata hii nitatekeleza Ilani ya CCM na mkakati wangu mwingine nitawakabidhi gari kwa ajili ya kubebea maiti na kusafirisha misiba .

Akielezea wimbi la kupokea wanachama kutoka vyama vya upinzani amesema, jana wamepokea wanachama 20 kutoka chama cha wananchi CUF Kariakoo Mtaa wa Mtambani na Juzi wamepokea wanachama 70 kutoka Mtaa wa Majengo tawi Geto Boys na kufanya jumla ya wanachama 90 ndani ya mwezi mmoja ambao wamerudi CCM kuunga mkono juhudi za chama hicho.

Kwa upande wake Kada wa CCM Philipo Mpemba amewataka wagombea wa vyama vya upinzani katika Jimbo la Segerea wanapokuwa Jukwaani watoe sera za vyama vyao wasingilie maisha ya watu sio vizuri.

Mpemba amesema, wagombea wa CCM wanapokuwa jukwaani wanatoa sera za chama hicho na kuelezea utekelezaji wa Ilani aijawai kuwachafua wapinzani.