Na Daud Magesa,TimesMajira Online,Mwanza
CHANGAMOTO ya usafiri iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, imepata mwarobaini baada ya Serikali kununua na kukamilisha ujenzi wa kivuko kipya cha MV Ukara II kwa gharama ya sh. bilioni 4.2.
Kivuko hicho ni ahadi ya Rais Dkt.John Magufuli,aliyoitoa baada ya Septemba 2018 kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere, kilichokuwa kikitoa huduma ya usafiri kati ya Bugorola Ukerewe na Bwisya Ukara na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Elius Mwakalinga amesema kivuko cha MV Ukara II ‘Hapa Kazi Tu’ kimeshushwa majini kwa majaribio ya kuona uwezo wake na kitaanza kazi baada ya majaribio hayo ya siku tatu, kwani masuala muhimu ya msingi yamekamilika.
“Kinachofayika hapa ni kuona uwezo wa kivuko kwa sababu hatutaki kuona maafa yanajirudia kwa wananchi watakaokitumia na tusingependa itokee kinyume na matarajio ya serikali, baada ya kivuko kuanza kutoa huduma,” amesema Mwakalinga.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Japheth Masele amesema ujenzi wa kivuko hicho kati ya vinne vipya ni ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano, ili kiwahudumie wananchi wa Kisiwa cha Ukara baada ya kuzama kwa MV Nyerere ahadi ambayo imekamilika.
Amesema kivuko hicho, kitakuwa ukombozi kwa wananchi wa Ukara baada ya kukamilika kwa kazi muhimu ya uhakiki uwezo wa kivuko, itakayofanywa na wataalamu kutoka Chuo cha Bandari (DMI) na Shiriki la Uwakala wa Meli (TASAC), ambalo litatoa kibali ili kianze kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi wa Ukara.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,John Mongela amesema maono na maagizo ya Rais Magufuli yametekelezwa ndani ya miaka miwili, baada ya ajali mbaya ya kuzama kwa MV Nyerere.
Amesema kukamilika kwa kivuko cha MV Ukara II ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo katika sekta ya usafiri wa majini, inaonesha serikali inavyowajali wananchi na kusikiliza matatizo yao na kuyatatua pamoja na kuhakikisha usafiri huo unakuwa salama na gharama nafuu.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano, imedhamiria kuufanya Mkoa wa Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa ukanda wa nchi za maziwa na hivyo, vivuko vinavyojengwa vitakuwa msaada mkubwa wa maendeleo na uchumi wa nchi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport (SMT), Major Songoro alisema uwekezaji wa serikali kujenga vyombo vya usafiri wa majini na kutoa kazi za ujenzi wa vivuko kwa wazawa, kutasaidia kujenga uwezo wa ndani tofauti na kazi hiyo kufanywa na kampuni za kigeni.
Akizungumzia kivuko hicho Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Colner Maghembe amesema wananchi wa Kisiwa cha Ukara, wanakisubiri kwa hamu kubwa kivuko cha MV Ukara kwani walikuwa na changamoto kubwa ya usafiri baada ya kuzama kwa MV Nyerere.
Pia amesema kukamilika kwa kivuko hicho, kutafungua uchumi wa Ukerewe na kuishukuru serikali kwa kutimiza ahadi ya kujenga kivuko kwa wananchi wake, huku akieleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya 2020/25 inaeleza kutajengwa meli itakayotoa huduma ya usafiri kati ya Ukerewe na visiwa vya Gana, Kamasi na Ukara.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu