December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kujisaidia porini kwa wakulima wa mpunga SALIOTA watoa neno

Na Esther Macha,Timesmajira,Online, Mbarali

UKOSEFU wa vyoo katika mashamba makubwa ya mpunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya umechangia wakulima kujisaidia vichakani hali inayopelekea kuwepo kwa kuzagaa kwa taka katika mashamba hayo na kusababisha uharibifu wa mazingira.

Hata hivyo imeleezwa kuwa uchafuzi huo wa mazingira umekuwa ukichangiwa na matumizi ya viatilifu shambani ambayo ni makopo ya sumu yaliyotumika yanayotakiwa kukusanywa na kuhifadhiwa katika vizimba ili kuepusha uchafuzi wa ardhi na vyanzo vya maji .

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Raphael Shitindi

Hayo yamesemwa Juni 2,mwaka huu na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali,Ofisa Mazingira wa Halmashauri hiyo, Raphael Shitindi wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa uhifadhi wa vyanzo vya maji ,mazingira na utalii Kanda ya Nyanda za Juu kusini ambapo kongamano hilo linaendeshwa na shirika lisilokuwa la kiserikali ambalo linalojihusisaha na masuala ya mazingira (SALIOTA).

Kongamano hilo la siku tano linafanyika uwanja wa shule ya msingi Majenje iliyopo kata ya Igurusi wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Shitindi amesema kuwa mashamba yote makubwa ya mpunga yanatakiwa kuwa na vyoo vitakavyosaidia kuepusha uchafuzi wa mazingira ambao umekuwa ukizagaa katika mashamba hayo.

Diwani Kata ya Igurusi Hawa Kihwele

“Pia ndugu zangu tuvipe ushirikiano vikundi ambavyo vinajuhusisha na shughuli za uondoaji taka ngumu katika makazi yetu na maeneo ya biashara ,shughuli mbali mbali zinapofanyika kwenye mashamba kunakuwepo na kundi kubwa la watu mashambani hivyo ni lazima kuwe na vyoo ambavyo vina umuhimu mkubwa “amesema.

Hata hivyo Shitindi amesema ukosefu wa kipato unafanya jamii kuvamia misitu na kufanya kilimo cha vinyungu na kulima kandokando ya mito na vyanzo vya maji ambapo vitendo hivyo huharibu vyanzo maji .

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo kuwa na kiserikali linalojihusisha na masuala ya mazingira (SALIOTA),Elisha Mwanikawaga amesema mashamba mengi hayana vyoo hali ambayo ni hatari kubwa na wilaya hii kuna baadhi ya wakulima wana mashamba makubwa ya mpunga kitendo cha kutokuwa na vyoo kinahatarisha usafi wa mazingira kwenye mashamba hayo.

“Wakulima wanapopiga dawa makopo wanaacha kwenye mito, bila kukusanya hivyo taasisi yetu iliona hili hivyo tuna uwezo tena wa kuanza kutoa elimu upya kwa wakulima kuona umuhimu wa kujenga vyoo kwenye mashamba ili kuendelea kulinda mazingira pamoja na vyanzo vya maji “amesema Shitindi.

Akielezea zaidi Mkurugenzi huyo wa SALIOTA amesema hali ya utupaji taka ovyo bado ni tabia ambayo jamii haijaweza kubadilika kwa kiasi kikubwa hivyo miji mingi imekuwa michafu na kusababisha milipuko ya magonjwa ya binadamu ,mifugo na wanyama pori.

Baadhi ya wadau walioshiriki kongamano hilo

Pia matumizi ya viwatilifu au sumu za kuulia wadudu na magugu katika maeneo ya mashamba lakini utunzaji wa vifungashio umekuwa changamoto.

Diwani wa Kata ya Igurusi ,Hawa Kihwele amesema kuwa uwepo wa kongamano hilo unasaidia wananchi kukumbuka uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao.

Hivyo hata uchafuzi wa mazingira unaofanyika kwenye mashamba ya mpunga kupitia kongamano hilo wakulima wataamka na kuona umuhimu wa kujenga vyoo kwenye mashamba yao ambako kunafanyika shughuli za kilimo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mji Mwema Kata ya Igurusi Esther Mtafya amesema kuwa wakulima wa Mbarali wanapoenda shambani wamekuwa wakijisaidia porini kutokana na ukosefu wa vyoo hivyo ni vema wakulima wote wenye mashamba kuwa na vyoo ili viweze kuwasaidia kipindi wakiwa kwenye shughuli zao za kilimo.