mwandishi: Ismail Mayumba
Nywila ni msimbo wa siri unaotumiwa kuthibitisha utambulisho wa mtu au kuruhusu ufikiaji wa mfumo wa kidijitali kama vile simu, kompyuta, barua pepe, akaunti ya benki mtandaoni, au mitandao ya kijamii.
Mifumo hii yote huhitaji mtumiaji kuweka nywila yenye nguvu yaani, nywila ngumu kubashiri inayochanganya herufi kubwa na ndogo, namba, na alama maalum. Hata hivyo, changamoto kubwa kwa watumiaji wengi ni kusahau nywila hizo kutokana na ugumu wake.
Kwa sababu hiyo, watu wengi wameamua kuzihifadhi nywila kwenye simu zao ili waweze kuzifikia kwa urahisi wanapozihitaji. Ingawa njia hii ni rahisi na inawasaidia watu, pia imekuwa fursa kubwa kwa wadukuzi na wahalifu wa mitandaoni.
Mfano Halisi wa Hatari Hii
Kuna kisa cha kweli kilichonisimuliwa na mhanga mwenyewe. Alipoteza simu yake bila kujua imeangukia wapi. Kwa bahati mbaya, hakuwa ameweka screen lock. Simu hiyo ilikuwa imevalishwa kasha lililokuwa na kadi ya benki ndani yake. Watu waliokota simu walifungua simu, wakakuta nywila za akaunti ya benki zilizohifadhiwa humo, na wakaenda kutoa pesa benki. Bahati nzuri kiasi kilichoibiwa kilikuwa kidogo, lakini tukio hilo lilimuumiza sana. Alienda benki kubadilisha nywila, lakini tayari alikuwa ameshaathirika. Je, ingekuwaje kama pesa zilizoibiwa zingekuwa nyingi?
Je, Nywila Zihifadhiwe Wapi?
Zipo njia mbalimbali za kuhifadhi nywila, lakini kila njia ina hatari yake. Njia bora zaidi na salama zaidi ni kuhifadhi nywila kichwani, na kuzoea kuikumbuka unapokuwa unajiandikisha au kuitumia mara kwa mara.
Nywila ni mlango wa taarifa zako binafsi na mali zako. Usiache mlango huo wazi. Hifadhi nywila kichwani mwako. Linda nywila zako. linda usalama wako.
More Stories
Dkt.Jingu ahimiza matumizi ya TEHAMA katika malezi
Bil.64.5 zimetengwa kwajili ya kupanga,kupima na kumilikisha ardhi halmashauri 131 nchini
LATCU Katavi yasaidia mahitaji ya Mil.5.7 kituo cha watoto yatima,mahabusu