December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kufungasha vyakula katika magazeti ni hatari, wino watajwa kusababisha saratani

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Mamlaka ya Chakula na Viwango (FSSAI) nchini India imebainisha kuwa, kufungasha vyakula katika magazeti ni hatari kwa afya kwani wino uliotumika unahusisha kemikali ambayo ina madhara kiafya ikiwemo kusababisha saratani.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo na kuchapishwa katika gazeti la kila siku la Hindustan Times, imesema kufungasha vyakula katika magazeti kunahatarisha maisha zaidi, hata kama chakula kimepikwa na kuiva kwa usafi wa hali ya juu.

Imeelezwa kuwa, wino wa kuchapia magazeti una rangi zenye madhara, lakini si tu kemikali hatari zilizomo katika gazeti, pia kuna vijidudu vinavyojukusanywa katika magazeti yaliyokaa muda mrefu ambavyo ni hatari kiafya.

Wataalamu kutoka ndani ya Mamlaka hiyo wamesema kuwa, hata maboksi yaliyotumika, au vitu vinavyotengenezwa kwa kutumia makaratasi yaliyotumika pia vina kemikali hatari ambazo zinaweza kuleta athari katika mfumo wa kusaga chakula ambavyo hutengeneza sumu hatari tumboni iwapo vitatumika kufungia au kubeba chakula.

“Rika lililo hatarini zaidi ni lile la Wazee, vijana wadogo, pamoja na watoto ambao maungo yao hayana uwezo wa kupambana na magonjwa, hivyo wako hatarini zaidi kupata saratani inayohusiana na ugumu wa maisha, haswa kama watakutana na vifungashio hatari kama hiyvo,” imeweka wazi taarifa hiyo.

Kufuatia athari hizo, Serikali ya India kupitia Waziri wa Afya, JP Nadda, imetoa maelekezo kwa mamlaka husika kutoka na mkakati wa kuzuia matumizi ya magazeti kama vifungashio vya chakula na bidhaa za chakula.