September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kuelekea uchaguzi serikali za mitaa,Jeshi la Polisi Mwanza lajipanga kudhibiti uhalifu

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27,2024,Askari wa Jeshi la Polisi zaidi ya 500, kutoka Wilaya za Mkoa wa Mwanza,wamepatiwa mafunzo maalumu ya kujiandaa kudhibiti matukio ya uhalifu kabla,wakati na baada ya uchaguzi huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbroad Mutafungwa,amesema matarajio ya jeshi hilo mkoani humo, ni kuona uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu,huku akiwataka Askari hao, kuzingatia mafunzo waliyopewa kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mutafungwa ametoa kauli hiyo, Septemba 2.2024,wakati akifunga mafunzo ya utayari yaliyofanyika kwa kipindi cha mwenzi mmoja,katika uwanja wa Polisi Mabatini, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.

Kwa upande wake Mkuu wa Oparesheni Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Aloyce Nyantora,amesema lengo la mafunzo hayo ya utayari,ni kumuwezesha Askari kuwa na utayari, ujasiri,umahiri, weledi na ukakamavu wa kumudu,ili kufanya majukumu yao ipasavyo.

ACP. Nyantora, amesema, mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi Agosti,1,2024,ambayo yamehusisha maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali.

Mbali na mafunzo ya medali za kivita.Pia Askari hao wamefundishwa mafunzo ya kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajia kufanyika Novemba 27, 2024.