November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kuelekea miaka 60 ya JKT,mafanikio lukuki yatajwa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limeelezea mafanikio yake linapoelekea kutimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake huku likitaja Moja ya mafanikio ni kuchangia katika Pato la Taifa kwa kutoa gawio Serikalini kupitia Shirika lake la uzalishaji Mali la SUMA JKT na hivyo kuiwezesha Serikali kuendelea na shughuli za maendeleo ikiwemo kujenga miradi ya kimkakati.

Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajab  Mabele ameyasema hayo leo Machi 3,2023 wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya miaka 60 ya JKT yanayotarajiwa kufanyika Julai 10 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi. 

Meja Jenerali Mabele amesema SUMA JKT ,kwa nyakati tofauti limeanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji Mali na huduma kupitia Sekta za ujenzi ,uhandisi na ushauri,sekta ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi ,sekta ya viwanda pamoja na sekta ya huduma na biashara lengo likiwa kujiongezea kipato huku akisema hatua hiyo imesaidia kupunguza mzigo wa kibajeti kwa Serikali wa uendeshaji wa shughuli za JKT ,miundombinu ya Makambi ya zamani Serikali imekuwa ikiyaboresha pamoja na kuanzisha Makambi  mapya bila kuathiri majukumu ya msingi.

“Jeshi la Wananchi wa Tanzania na  Taifa kwa ujumla linajivunia mafanikio ya JKT katika kutimiza Malengo yake kwa jamii na shughuli zake za kiuchumi ambapo kutokana na umuhimu wake katika Taifa ,JKT limeweka utaratibu wa kujitathimini wapi limetoka,lilipo na linapoelekea  kwa kipindi Cha miaka 10.”

Vile vile ameelezea  mafanikio mengine ya JKT ni kupitia kilimo mkakati ambacho kilianzishwa kwa ajili ya kuhakikisha JKT linajitosheleza kwa chakula huku akisema ili  kufikia azma ya kujilisha wameanzisha kilimo mkakati ambacho pamoja na changamoto za hali ya hewa hapa nchini ,lakini kwa sasa hawategemei kununua mahindi wala mchele kwa ajili ya kulisha vijana na kwamba  mkakati wao  ni kuhakikisha ifikapo 2024/2025 wanajilisha na kwamba hawana wasiwasi katika kufikia malengo hayo.

Kwa mujibu wa Meja Jenerali Mabele , kuelekea maadhimisho hayo JKT litafanya shughuli za kijamii ikiwemo kuchangia damu ,kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ikiwemo hospitali ,upandaji wa  miti ili kuendelea kuifanya Dodoma ya kijani na kutoa msaada wa kibinadamu kwa wahitaji .

Aidha Meja Jenerali Mabele amesema pamoja na utekelezaji wa shughuli zote hizo lakini pia JKT bado limeendelea na majukumu yake ya msingi ya malezi ya vijana ,uzalishaji mali na Ulinzi limekuwa likifanya maboresho mbalimbali ili kuendana na wakati pamoja na mabadiliko ya satansi na Teknolojia

Kwa upande wake Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT Brigedia Hassan Mabena amesema Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikiitumia Taasisi hiyo kuhakikisha vijana wanapata uzalendo,ukakamavu,mafunzo ya ujasiriamali,mafunzo ya ufundi stadi ambapo vyote kwa pamoja vinakwenda kuwasaidia wao katika kujiajiri na uendesha maisha yao.

Naye ,Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo Kanali George Kazaula amesema JKT limewaalika wadau mbalimbali kuelekea maadhimisho hayo kwa lengo la kuhakikisha yanafanyika kama yalivyopangwa.