December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba Mo Dewji, akimkabidhi jezi shabiki aliyechaniwa jezi ya simba na mashabiki wa Yanga Kindio Hassan. Katika sherehe ya siku ya Mwananchi iliyofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam

Kuchaniana jezi ni kero za mashabiki Simba, Yanga

Na Philemon Muhanuzi, Times Majira Online

SIKUSHANGAZWA kuiona video ya shabiki wa Simba akiwa ameduwaa baada ya mashabiki wa Yanga kumchania jezi yake siku ya Mwananchi. Ile ilikuwa ni siku maalum ya wanayanga kujidai na kuringia timu yao.

Ingawa haiwezi kuwa ni haki yao kumdhalilisha shabiki wa Simba kisa tu rangi ya fulana aliyoivaa. Masuala ya kudhalilishana ni ya kawaida sana pale Uwanja wa Taifa. Ni hulka ya siku nyingi haikuanza jana wala juzi.

Ni kielelezo tu cha uanamichezo wenye kupungukiwa ustaarabu wa kawaida kabisa. Mashabiki wa timu za Uingereza wanapokuwa na pombe kichwani ndipo vichwa vyao huwaka moto na kufanya mambo ya kipuuzi.

Lakini kama hawajawa na ulevi ndani ya damu zao, watakachokifanya kibaya ni matusi ya ishara kama vile kutumia kidole cha kati.

Watatungiana nyimbo za kumkera kocha ambaye timu yake imezidiwa uwanjani na kufungwa magoli mengi. Ni nadra sana kwao kuingiliana maungoni kisa shabiki mmoja kakatiza tena kwa upole mbele ya macho yao.

Mechi inapomalizika kila mmoja anaondoka kutoka eneo la uwanjani na kuelekea nyumbani kuendelea na shughuli zake nyinginezo. Zile mechi za kombe la dunia ni mwalimu wa uhakika wa ushabiki wa kiungwana.

Wanaonekana kwenye runinga mashabiki wa mataifa tofauti wakiwa wamevaa fulana za rangi tofauti lakini wakicheka pamoja na kujenga urafiki mpya. Hawana sababu ya kujenga uhasama wakati wanajua mechi inachezwa kwa muda wa saa moja na nusu na kumalizika.

Ni kero sana kumuona shabiki mgeni wa uwanja wa Taifa akiwa amevaa fulana yake ya rangi ya njano na kijani akisumbuliwa na mashabiki wa Simba kisa amekatiza katika eneo asilotakiwa kukatiza!.

Shabiki mgeni asiyejua lolote kuhusiana na utamaduni wa upande wanaokaa mashabiki wa Simba na wale wa Yanga, katoka mkoani na kaona ni bora aende uwanja wa Taifa ili akafurahie burudani. Halafu anapokolewa katika hali ya uonevu usio na msingi wowote akijikuta anachaniwa jezi.

Nimemuelewa Mohamed Dewji kwa kuamua kumpatia jezi mpya shabiki wa Simba aliyekutana na adha ya kuchaniwa jezi siku ya Yanga kutambulisha makocha na wachezaji wake wapya. Mo Dewji kaongozwa na ustaarabu wa kawaida tu wa kibinadamu.

Ingawa uamuzi wake huo ni sawa na kufikisha ujumbe wa masikitiko kwa watu wanaokwenda pale uwanja wa Taifa kutazama mechi za mpira wa miguu.

Uhuni wa shabiki kuchaniwa jezi umeweza kurekodiwa na simu ya mkononi na kusambazwa mitandaoni mpaka ikamfikia Mo Dewji, yapo mengi ya kijinga yanayofanyika pasipo kurekodiwa.

Yapo maudhi mengi sana yenye kuthibitisha ustaarabu mdogo wa baadhi yetu tunaokwenda viwanjani haswa pale uwanja wa Taifa.

Lipo kundi la wahuni wenye kujishughulisha na uuzaji wa bangi wanaokaa eneo la kuizunguka ile runinga kubwa ya kusini mwa uwanja.

Ukiwa umekaa chini ya runinga ile usawa wa nyuma ya goli la kusini mara nyingi tu upepo hukatiza na harufu kali ya bangi.

Kichwa chenye bangi mara nyingi hufanya maamuzi ya hatari kwani hakipo sawa, huwezi kukilinganisha na kichwa safi kisicho na madawa ya kulenya ya aina yoyote.

Na hii biashara ya bangi pia hufanyika katika jukwaa jipya la mzunguko la uwanja wa Uhuru. Imekuwa ni biashara inayopuuziwa na kuachwa iendelee kumbe ina madhara ya muda mfupi na mrefu kwa wanunuzi wa bangi.

Wanaochana jezi kwa sababu tu hazina rangi ile ile kama ya zile walizozivaa wao, pengine ni sehemu ya wateja ya bangi inayouzwa na watu wachache wenye kuharibu taswira nzima ya ushabiki ndani ya uwanja wa Taifa.

Mamlaka husika zinakumbushwa juu ya kusimamia viwango vya ubora wa ustaarabu ndani ya mojawapo ya viwanja bora kabisa katika ukanda huu wa Afrika.

Jezi za Simba na Yanga zinatengenezwa kila kukicha, zipo za bei kubwa na bei ndogo inategemea na pesa ya mnunuzi ipo vipi.

Lakini kuchaniana jezi eti kwa sababu haifanani na ile uliyovaa ni ushamba ambao unatia doa zile mbwembwe zetu za kishabiki.

Mo Dewji ameweza kumpatia jezi mpya ya Simba yule shabiki aliyekutana na adha za siku ya Mwananchi. Mojawapo ya lengo la maamuzi ya Mo Dewji ni kuonyesha kuwa Simba ni timu ya waungwana, ni jambo jema.

Lakini wanasimba wengi wakiwa katika upande wao wa uwanja wamekuwa na tabia zile zile za wale waliochania jezi yule shabiki wa Simba aliyepewa jezi mpya na Mo Dewji.

Kwa ujumla kuna kundi kubwa sana la mashabiki wenye tabia za hovyo zenye kutakiwa kukemewa kwa nguvu kubwa.