Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
BAADA ya kilio cha wananchi kutoka kwa makundi mbalimbali, hatimaye Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga imesitisha ujenzi wa vibanda vya biashara kwenye Uwanja wa Michezo Soko la Manundu.
Na badala yake fedha zilizokuwa zijenge vibanda hivyo, zitapelekwa kuboresha Banda la Soko Kuu la Manundu ambalo lilikuwa linatumiwa na wauza samaki.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 9, 2023 mara baada ya kikao cha Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe Francis Komba, alisema wamefikia maamuzi hayo kwa maslahi mapana ya halmashauri na wananchi wa Korogwe.
“Tumekubaliana kusitisha ujenzi wa vibanda vya biashara kwenye Uwanja wa Michezo uliopo Soko la Manundu, na badala yake fedha zilizokuwa zijenge vibanda hivyo, sasa tutaboresha banda lililopo ndani ya Soko la Manundu. Na ujenzi wa vibanda hivyo, ulikuwa tuanze na sh. milioni 30” alisema Komba.
Komba alisema pia amewapa watendaji hadi mwezi mmoja wawe wamekamilisha mchakato wa kuwapeleka Wamachinga kwenye eneo la wazi kwa Sheikh Ramia ili wafanye shughuli zao hapo badala ya kuzagaa kwenye mji mzima wa Korogwe.
“Mkurugenzi na Watendaji wake wamesema watawakusanya na kuwahamisha Wamachinga wote waliopo hapa mjini Korogwe na kuwapeleka eneo la kwa Sheikh Ramia baada ya wiki mbili, lakini mimi nimewapa mwezi mmoja, ili wasije wakasema wamekwama mahali” alisema Komba.
Komba pia alimpongeza Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha za miradi sh. bilioni 3.2 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye sekta za elimu, afya, maji, barabara na shughuli nyingine.
Baadhi ya wananchi wa Mji wa Korogwe akiwemo Ibrahim Abdillah, walikuwa wanahoji imekuwaje Halmashauri ya Mji Korogwe imeamua kujenga vibanda kwenye uwanja wa michezo ikiwemo mpira wa miguu kwenye Uwanja wa Manundu Sokoni, kwani kufanya hivyo, ni kuwakosea wananchi wa Korogwe.
“Uwanja wa Michezo Manundu unafanyiwa vitu vingi ikiwemo mpira wa miguu na Serikali kufanya shughuli zake. Tulishangaa kuona Halmashauri ya Mji Korogwe inaua huo uwanja na kujenga vibanda. Bahati nzuri Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji, Komba amesitisha zoezi hilo la ujenzi. Tunaomba Serikali kuyatunza maeneo ya wazi” alisema Abdillah.
Abdillah, pia alishangazwa na eneo lililotengwa kwa ajili ya Wamachinga pale kwa Sheikh Ramia kushindwa kufanya kazi wakati choo kimeshajengwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Hivyo ameitaka Serikali kuwa na utekelezaji kwenye miradi yake ya maendeleo.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito