Na Mwandishi wetu,Pwani
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, leo tarehe 18 Desemba 2024, amefungua rasmi Kongamano la Uwekezaji na Biashara la Mkoa wa Pwani, akitoa pongezi kwa jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Naibu Waziri Nyongo alieleza kuwa Serikali imechukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya biashara, ikiwa ni pamoja na kufuta au kupunguza jumla ya tozo na kodi 374 ambazo zilikuwa kikwazo kwa wafanyabiashara. Aidha, alibainisha maboresho ya mifumo ya kidijitali, kama vile Mfumo wa Kielektroniki wa Uwekezaji wa Tanzania (Tanzania Electronic Investment Window – TelW), ambao umelenga kurahisisha huduma kwa wawekezaji na kuongeza ufanisi.
Naibu Waziri Nyongo aliwataka wawekezaji kutambua fursa za kipekee zilizopo katika Mkoa wa Pwani, ambazo zinajumuisha miundombinu bora, nishati ya uhakika, na ukaribu wake na soko kubwa la Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa Mkoa wa Pwani ni sehemu muhimu kwa uwekezaji, hasa kwa viwanda, kilimo, na sekta nyingine zinazochangia maendeleo ya taifa.
Kongamano hilo limebeba kaulimbiu inayosema, “Wekeza Pwani: Sehemu Sahihi kwa Uwekezaji”, ikilenga kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje kwa lengo la kuimarisha uchumi wa taifa kupitia sekta mbalimbali.
Aidha, Naibu Waziri alitoa wito kwa wadau wote kushirikiana kwa karibu katika kuvutia wawekezaji na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya uwekezaji, viongozi wa serikali, na wawekezaji, likiwa ni jukwaa muhimu la kujadili na kubuni mbinu bora za kuendeleza uwekezaji nchini.
More Stories
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang
Daktari Dar ajishindia Mil. 100/- za Fainali NMB Bonge la Mpango