October 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kongamano la 10 Jotoardhi kufanyika Tanzania kuanzia Oktoba 21

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC)pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maziringira (UNEP),inaandaa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) litakalofanyika nchini Tanzania kuanzia tarehe 21-27 Oktoba, 2024 huku washiriki zaidi ya 700 wakitarajiwa kushiriki.

Kongamano hilo litafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, linalotarajiwa kuwa na washiriki takribani 700 mpaka 1000 na kuzifunguliwa na Dkt.Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,likiwa na kaulimbiu inayosema, “Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi katika Afrika, Masoko ya Gesi ya Ukaa na Upiunguzaji wa Gesi ya Ukaa”.

Hayo yamesemwa jijini hapa jana na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC),Mhandisi Mathew Mwangomba
ambapo alisema kuwa Kaulimbiu hiyo inasadifu kwa kiasi kikubwa adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia, kama ilivyoanishwa katika mkakati aliouzindua mapema mwezi Aprili, 2024 wenye lengo la kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.

Mha.Mwangomba amesema kuwa Kongamano hilo litaangazia mada kama uzalishaji wa umeme kwa kutumia jotoardhi (Geothermal),Matumizi ya moja kwa moja ya jotoardhi katika sekta kama kilimo na ufugaji hasa wa samaki, Uhandisi wa visima vya jotoardhi na teknolojia mpya,
Njia za kupata ufadhili wa miradi ya nishati mbadala ikiwemo nishati ya jotoardhi,Uchambuzi wa faida za kimazingira na kijamii katika maendeleo ya miradi ya jotoardhi,Utafiti na uendelezaji wa Rasilimali za Jotoardhi,Sera na udhibiti katika sekta ya Rasilimali ya Jotoardhi na faida ya Kimazingira na kijamii katika maendeleo ya Miradi ya jotoardhi.

Aidha ametaja faida za Kongamano hilo kwa washiriki kuwa ni wa Kongamano wa ARGeo-C10 watafaidika kwa kupata Elimu na Maarifa,Mtandao wa Kitaaluma,Fursa za Biashara, Ziara za Mafunzo,Ufahamu wa Sera na Masoko,kukuza Uwezo na kupata Maarifa ya Kimataifa.

Amesema kuwa kongamano hilo limegawanyika katika programu ambazo ni Oktoba 21-22 2024 ni Kozi fupi,Oktoba 23-25, 2024 ni Mkutano Mkuu na Oktoba 26-27 2024 ni Ziara ya kitalii na kisayansi katika miradi ya jotoardhi ya Mbeya-Ngozi na Songwe – Songwe.

Vilevile Mhandisi Mwangomba amesema kuwa Kongamano hilo litafungwa Oktoba 25, 2024 na Kassim Majaliwa Majaliwa,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo alisema Kwa usajili na maelezo zaidi,wanaweza tembelea tovuti rasmi ya ARGeo-C10 ambayo ni https://theargeo.org/C8/c10-registration.html.

Hata hivyo Mhandisi Mwangomba ameeleza kuwa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambayo inamilikiwa na serikali ya Tanzania kwa 100% iliyoanzishwa tarehe 19 Desemba 2013 kwa lengo la kuendeleza rasilimali ya jotoardhi (geothermal) nchini na kuanza rasmi shughuli zake tarehe 1 Julai, 2014.

“Kazi yake ni kufanya utafiti, maendeleo, na uendeshaji wa miradi ya nishati ya jotoardhi. Miradi hii inalenga kuzalisha nishati safi ya umeme wa gharama nafuu na endelevu kutokana na nishati ya jotoardhi ambayo inapatikana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania,”amesema.

Amesema Jotoardhi (geothermal) ni aina ya nishati mbadala ambayo inatokana na joto lililoko chini ardhini.