November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kocha Thomas: Tumejifunza, tunarudi kujipanga

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KOCHA wa mchezo wa riadha anayewanoa nyota mbalimbali hapa nchini akiwemo Failuna Abdi na Gariel Geay, Thomas Tlanka amesema kuna vingi wanatakiwa kufanya kama makocha ili kuhakikisha wanariadha wa Tanzania wanafanya vizuri katika mbio mbalimbali za Kimataifa wanazokwenda kushiriki.

Kocha huyo ametoa kauli hiyo baada ya mwanaridha kutoka nchini Kenya, Kibiwott Kandie Kuvunja rekodi ya Dunia katika mbio za kilometa 21 za Valencia iliyokuwa ikishikiliwa na Geoffrey Kamworor aliyetumia muda wa dakika 58:01 katika mbio za mbio za IAAF Gold Label akivunja rekodi ya Abraham Kiptum ya aliyetumia dakika 58:18 nchini Hispania mwaka uliopita.

Lakini rekodi hiyo imevunja siku chache zilizopita na Kandiye ambaye alitumia dakika 57:32 na kuweka rekodi mpya ya dunia ya mbio za Kilometa 21 katika mbio za Valencia ‘Valencia Half Marathon’.

Mbali na Kandie rekodi ya Kamworor pia rekodi hiyo ilivunjwa na Mganda Jacob Kiplimo aliyemaliza nafasi ya pili akitumia dakika 57:37, Rhonex Kipruto alikuwa wa tatu akitumia dakika 57: 49 huku Alexander Mutiso akitumia dakika 57: 59.

Katika mbio hizo Wakenya Philemon Kiplimo alitumia dakika 58:11, Kelvin Kiptum alitumia dakika 58:42 huku mkenya mwingine Bravin Kiptoo akitumia dakika 59:37 huku Julien akishika nafasi ya nane akitumia dakika 59:55, Carlos Mayo alitumia saa 1:00:06 huku Mtanzania Gabriel Geay akitumia saa 1:00:40.

Akizungumza na Mtandao huu kocha Thomas amesema kuwa, mashindano hayo yamewaonesha ni wapi walikosea katika maandalizi na wanapotakiwa kupaweka sawa kabla ya kwenda mbio nyingine za Kimataifa.

Amesema, kwanza mashindano hayo yalikuwa makubwa na magumu na kwani yameshirikisha wanariadha wakubwa Duniani tofauti na wengi walivyofikiria na ndio maana wanariadha wanne wamevunja rekodi ya dunia.

Amesema kuwa, yeye kama kocha anampongeza Geay kwa kushika nafasi hiyo ya 10 kwani si haba na pia ni historia kwake na wanaamini atapambana zaiidi ili kupanda zaidi kiwango na kushika nafasi za juu kabisa ikiwa atashiriki mbio nyingine za kimataifa.

Amesema, mashindano hayo yamempa funzo kuwa ili kuwa bora na kuweza kumudu ushindani wa kimataifa basi ni lazima upambane kufanya mazoezi ya kutosha ili kuweza kupambana zaidi na kupeperusha vema bendera ya nchi.

“Kupitia mashindano haya tumejifunza kuwa hatutakiwi kuchukulia mambo kirahisi kwani kutokana na janga la Corona tulijua wanaridha wengi hawatashiriki lakini leo tumeona kupitia mashindano haya rekodi ya Dunia kwa mbio za kilometa 21 imevunjwa na wanariadha wanne hivyo ni wazi tunapaswa kujipanga zaidi hasa katika maandalizi ili kuwa bora na kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo, ” alisema kocha Thomas.

Akizungumzia kauli iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi ya kutaka mashirikisho na vyama mbalimbali vya michezo nchini ambavyo vinasimamia timu za Taifa kuwasilisha ratiba na mikakati ya timu hizo kwa mwaka 2021 kabla ya mwaka huu kumalizika, kiongozi huyo amesema kuwa, jambo hilo linadhihirisha kuwa Serikali imepania kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya michezo.

Amesema, kwa mujibu wa kalenda tayari mikakati yao ilishaandaliwa kwani inaanza Novemba hivyo kitu pekee wanachokiomba ni Shirikisho la Riadha (RT) kuingiza mikakati mizuri zaidi ambayo pia itawabeba wanaridha wengine wanaokwenda kupeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya kimataifa.

Amesema, wao kama wadau wanaamini ikiwa mikakati hiyo itajadiliwa kwa kina na RT kabla ya kuiwasilisha wizarani kuna uwezekano idadi ya wanariadha wa timu ya Taifa wanaokwenda kuiwakilisha nchi kimataifa ikaongezeza na kuwa chachu ya kuanza kufanya vizuri zaidi na kuitangaza nchi.