November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kocha Simba na Wenzake wanaswa na Dawa za kulevya.

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) Gerald Kusaya ametangaza Watuhumiwa 9 wakiongozwa na Mmiliki wa Kambiaso Sports Academy, Alhaj Kambi Zubeir Seif pamoja na Kocha wa Makipa wa Klabu ya Simba, Mwalami Sultan kuhusika kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya Heroin yenye jumla ya Kilo 34.89.

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya amesema leo kuwa Mamlaka hiyo imekuwa ikifanya operesheni maeneo mbalimbali nchini kuanzia Oktoba hadi Novemba mwaka huu na kufanikiwa kukamata watuhumiwa wengu wanaojihusisha na biashara ya dawa 

Kusaya amewataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo ni Kocha wa Makipa wa Simba Muharam Said Sultani(40) mkazi wa Kigamboni na kufafanua kwamba Muharam amewahi pia kuichezea timu ya Simba.

Wengine ni Mfanyabiashara na Mmiliki wa Kituo cha Soka cha Kambiasso Sports Academy kilichopo Tuangoma wilayani Kigamboni Alhaj Kambi Zeber Seif maarufu kwa jina la Kambiasso au Alhaj Kambi.Alhaj Kambi mbali ya kumiliki kituo hicho cha soka ana miliki kampuni ya Safia Group of Companies inayomiliki magari ya kusafirisha abiria (daladala) kutoka Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Pwani.

Pia Mamlaka hiyo inamshikilia Said Abeid Matwiko ambaye anaishi Magole A Kivule na kazi yake ni fundi selemala,mwingine ni Maulid Mohamed Mzungu maarufu kwa jina la Mbonde (54) mkazi wa Kisevule ambaye kazi yake ni mkulima.

Amewataja watuhumiwa wengine ni John Andrew John (40) mkazi wa Magore – Kitunda ambaye ni mfanyabiashara na amekuwa na jukumu la kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka kituo cha Soka Kambiasso .Pia wanamshikilia Seleman Matola Said(24) mkazi wa Temeke –Wailes .Matola ni mtoto wa dada yake na mtuhumiwa Alhaj Kambi.

Mwingine ni Hussein Mohamed Pazi(41) mkazi wa Kibugumo wilayani Kigamboni ambaye ni mfanyabiashara na mtuhumiwa wa tisa ni Ramadhan Rashid Chalamila(27)ambaye ni mfanyabiashara. “Watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.”

Katika tukio lingine, Kamishina Jenerali Kusaya amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inamshikilia mtuhumiwa Abdulnasir Haruon Kombo(30) mfanyabiashara  na mkazi wa Kaloleni jijini Arusha akiwa na biskuti 50 zinazotengenezwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi kama moja ya malighafi akiwa anaziuza katika eneo la Kaloleni.

“Aidha kuhusiana na tukio hili la ukamataji wa biskuti zenye bangi , tumefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine anayeitwa Hassan Ismail(25) mkazi wa Olasiti jijini Arusha.”amesema.
 Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya.