January 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KMC wazitaka alama tatu za Azam

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

BAADA ya kuambulia alama mbili katika mechi zao mbili zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) benchi la ufundi la timu ya KMC limesema sasa wanahamishia nguvu katika mchezo wao ujao wa ugenini dhidi ya Azam FC utakaochezwa Mei 15.

KMC wataingia katika mchezo huo utakaochezwa saa 1:00 katika uwanja wa Azam Complex huku wakitaka kulinda ushindi wao wa mzunguko wa kwanza ambapo walifanikiwa kuwachapa Azam goli 1-0 katika mchezo uliochezwa Novemba 21 goli kilifungwa dakika ya 57 na Reliant Lusajo ambaye kwa sasa anaitumikia timu ya Namungo FC.

Akizungumzia maandalizi yao yatakayoanza rasmi leo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala amesema kuwa, kufuatia sare ya bila kufungana waliyoipata katika mchezo wao wa juzi dhidi ya Namungo, leo benchi lao la ufundi litaanza rasmi na programu yao mpya kuelekea mechi na Azam.

Amesema, bechi lao la ufundi limeweka wazi kuwa kazi kub wa iliyo mbele yao kwa sasa ni kurekebisha makosa yaliyowanyima alama tatu katika mchezo wao uliopita ili kuchukua alama tatu ambazo zitawasogeza katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.

Amesema, ukiangalia katika msimamo wapinzani wao wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 54 hivyo ni ngumu kuwashusha jambo litakalofanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi.

Licha ya ugumu katika mchezo huo lakini watawaandaa vijana wao kwa ajili ya kupambana kwa hali na mali na kutumia makosa yatakayoyafanya wachezaji wa Azam kuwapa alama tatu muhimu.

“Leo tunaanza rasmi maandalizi kuelekea mechi dhidi ya Azam ambayo yatatuhakikishai kuchukua alama tatu nyingine kwa Azam, tayari viongozi wetu wa benchi la ufundi wameshaandaa program maalum ambayo tunaamini itafanikiwa kutupa kile tunachokihitaji,” amesema Christina.