Na Penina Malundo,Timesmajira
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Nurdin Babu amezindua rasmi Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa lengo ya kusaidia kupunguza migogoro ya wananchi dhidi ya Serikali huku kuwawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia Utawala wa Sheria na kushirikiana kwa ukaribu na Wadau pamoja wananchi katika kutatua masuala ya Kisheria.
Akizungumza leo mkoani humo wakati wa ufunguzi rasmi wa Kliniki hiyo Mkuu wa Mkoa huo, ameipongeza na kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Kilimanjaro katika utoaji wa huduma ya Kliniki bure kwa wananchi wa Kilimanjaro.
Amesema utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa mkoa huo inaonyesha namna Ofisi hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilivyojikita kusogeza huduma kwa wananchi hususani kwenye maeneo mbalimbali nchini.
“Leo tunakwenda kuanza Kliniki ya Sheria ni matumaini yangu itawasaidia wananchi wenye matatizo ya kisheria kutatuliwa changamoto zao mbalimbali kupitia timu nzuri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,”Amesema
Aidha ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kushiriki kwa wingi katika Kliniki hiyo ili wapate suluhu ya changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili.
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tamari Mndeme amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vyema kutoa huduma za kisheria bure kwa wananchi kupitia Kliniki hiyo.
“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kuwahudumia Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na tuna wataalamu wa kutosha tunaamini kupitia Kliniki hii changamoto mbalimbali za wananchi zitatatuliwa,”amesema Tamari.
Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ni mwendelezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusogeza huduma za Kisheria kwa Wananchi.
Uzinduzi huo, utafuatiwa na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi ambapo inafanyika kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Huduma hizo zitatolewa katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi Moshi Mkoani Kilimanjaro kuanzia Januari 21 hadi 27, 2025.
More Stories
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba
Majaliwa:Serikali imefanya uwekezaji mkubwa TMA