Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
KATIKA kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya vyama vya ushirika nchini, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) kimeanzisha kliniki maalumu itakayochochea weledi na ufanisi wao.
Mratibu wa Kliniki hiyo ya Maendeleo ya Ushirika Bahati Rukiko akiongea na gazeti hili katika mahojiano maalumu yaliyofanyika hivi karibuni kwenye maonesho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) Mkoani Tabora na kubainisha kuwa programu hii mkombozi kwa wanaushirika wote.
Anabainisha kuwa sekta ya ushirika na vyama vya ushirika kwa ujumla vimekuwa vikipitia changamoto mbalimbali kutokana na ukosefu wa huduma sahihi za usaidizi (cooperative support services) hivyo kushindwa kujiendesha kibiashara.
Anaongeza kuwa ukosefu wa huduma za usaidizi kwa vyama hivyo umepelekea kukosekana usimamizi thabiti na wenye ufanisi kwa mali za vyama vya ushirika na maendeleo yao hivyo kusababisha vyama hivyo kupata hasara na vingine kushindwa kujiendesha.
Anasisitiza kuwa awali huduma za usaidizi kwa vyama hivyo zilikuwa zikifanyika kwa njia ya semina, warsha pamoja na ziara za mafunzo lakini njia hizo zimekuwa zikiwanyima wanaushirika fursa ya kupata huduma toshelevu kwa masuala yao.
Rukiko anafafanua kuwa kutokana na hali hiyo Chuo Kikuu Cha Ushirika (MoCU) kupitia Taasisi ya Elimu Endelevu ya Ushirika (ICCE) kimeamua kuanzisha mfumo wa utoaji huduma za usaidizi kwenye vyama vya ushirika kupitia Kliniki ya Maendeleo ya Ushirika (KMU) ili kuharakisha utatuzi wa changamoto zao.
‘Kliniki hii ni moja ya njia za kisasa zenye ufanisi katika kutatua kwa wakati changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika nchini itakayopeleka wanaushirika kunufaika zaidi’, alisema.
Anaongeza kuwa kliniki hii siyo ya afya bali ni moja ya njia za kutoa huduma za ana kwa ana kati ya mshauri na mshauriwa ili kuwezesha wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika kujifunza namna ya kutatua changamoto zinazokabili vyama vyao.
Mratibu anabainisha kuwa Kliniki hii itaendeshwa kwa njia 2 ya kwanza ni ya ana kwa ana na ya pili ni ya kidigitali, akaongeza kuwa kliniki ya ana kwa ana itaendeshwa kwa njia ya mikusanyiko ya wanaushirika kama vile majukwaa ya ushirika na maonesho au gari linalotembea (mobile clinic).
Na Kliniki ya kidigitali itaendeshwa kutumia mfumo maalumu wa komputa au simu za mkononi ambapo mshauriwa ataongea moja kwa moja na mshauri na kupewa huduma ya usaidizi itayosaidia kutatua changamoto zao.
Manufaa ya Kliniki ya Maendeleo ya Ushirika Naye Mkuu wa Idara ya Manunuzi na Ugavi wa Chuo hicho, Dkt Faustine Panga anaeleza kuwa Kliniki ya Maendeleo ya Ushirika ni mwarobaini wa utatuzi wa changamoto zinazokwamisha ufanisi wa vyama vya ushirika nchini.
Anabainisha kuwa kupitia Kliniki hii, wataalamu wa Chuo Kikuu Moshi (MoCU) watatumia ujuzi, uzoefu na umahiri wao kutoa ushauri wa kitaalamu wa mambo yote yanayokwamisha maendeleo ya vyama vya ushirika ili kupiga hatua zaidi.
Anasema huduma hii inatoa nafasi ya mawasiliano ya moja kwa moja na mtoa huduma hivyo kutoa fursa kwa wanaushirika kueleza changamoto zao moja kwa moja na kupata ushauri wa kitaalamu kupitia Kliniki hii ambayo pia hujulikana kama Cooperative Development Clinic (CDC).
Dkt Faustine anabainisha lengo kuu ya huduma hii kuwa ni kutatua changamoto zozote zinazovikabili vyama vya ushirika na kuwapa ushauri wa nini wanapaswa kufanya ili kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Anatoa wito kwa wanaushirika kuchangamkia huduma hii kwa wingi zaidi ili shughuli wanazofanya ziwe na tija zaidi ili kujiongezea kipato na kuinuka zaidi kiuchumi.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia