December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiwanda cha TPPL chatoa msaada wa vifaa tiba

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira,Online Tanga

KIWANDA cha Tanga Pharmaceutical and Plastic Limited (TPPL) kimetoa msaada wa vifaa tiba katika kituo cha Afya Pongwe Jijini Tanga wenye thamani ya sh. milioni 2.4 kwa ajili ya kusaidia kambi ya upasuaji wa pua, masikio na koo.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo,Afisa Rasilimali Watu wa Kiwanda hicho, Jenipher Mburuja amesema kiwanda hicho kimetoa msaada huo ikiwa ni katika kurudisha kwa jamii inayowazunguka ambapo wamekuwa wakifanya hivyo kwenye kusaidia masuala mbalimbali.

Amesema baada ya kupokea maombi ya ufadhili kwa ajili ya kambi ya upasuaji wa Pua,Masikio na Koo waliona ni muhimu kuwasaidia msaada huo wa vifaa ili kuweza kufanikisha kambi hiyo ikiwa ni kuondosha changamoto ambazo zinaweza kujitokeza wakati wakiendelea na zoezi hilo.

“Tulipopokea maombi ya ufadhili wa Kambi hiyo kwa ajili ya vifaa tiba vya upasuaji wa pua,masikio na koo na tukiwa kama wadau wa afya tukaona tununue vifaa hivi vyenye thamani ya milioni 2.4 kwa ajili ya kuwasaidia uponyaji wa magonjwa hayo,”” Amesema Mburuja ambaye ni Afisa Rasilimali Watu wa Kiwanda cha (TPPL)

Afisa Rasilimali Watu wa Kiwanda cha Tanga Pharmaceutical and Plastic Limited (TPPL) Jenipher Mburuja (kushoto) akimkabidhi msaada wa vifaa tiba Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Pongwe Dkt Ummykulthum Kipanga juzi kwa ajili ya kusaidia kambi ya upasuaji wa pua, masikio na koo katika halfa iliyofanyika kwenye kituo hicho. Kushoto anayeshuhudia ni Afisa Muuguzi wa Kituo cha Afya Pongwe Bahati Shiminogen, Picha na Oscar Assenga

Aidha amesema pia katika kurudisha kwa jamii inayowazunguka kiwanda hicho ambacho ni wadau wakubwa wa Elimu,Usalama na Afya,wametoa misaada mbalimbali kwa jamii ikiwemo kujenga banda la watoto la kliniki kituo cha Afya Makorora, Benchi la kukalia wagonjwa kituo cha Afya Duga,wamewakatia Bima ya Afya ya NHIF wanafunzi walemavu 83 Pongwe.

Afisa Rasilimali huyo amesema pia walikwisha kununua viti vya kusubiria wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo ikiwemo kutoa vitanda 20,magodoro 20 na shuka 20 katika kituo cha Afya Duga ikiwemo friji la kuhifadhia damu kwenye kituo cha Afya Pongwe.

Akizungumza wakati akipokea msaada huo Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Pongwe, Dkt .Ummykulthum Kipanga alishukuru kwa msaada huo ambao wamepatiwa na kiwanda hicho huku akieleza umefika wakati muafaka, kwani na Tanga kuna tatizo la Koo na Pua ambalo linapelekea watu kwenda Dar es Salam kwa ajili ya kufuata matibabu .

Amesema baada ya kuliona hilo waliwaomba madaktari bingwa wafike kwa ajili ya kufanya upasuaji kwenye kituo hicho na kiwanda hicho hakikuweza kuwaacha nyuma waliwashika mkono kufanikisha jambo hilo.

Naye kwa upande wake Afisa Muuguzi wa Kituo cha Afya Pongwe Bahati Shiminogeni alisema wamefurahi sana wao kama watumishi kwa vifaa hivyo hasa Jik ambayo ni gharama kubwa ukiangalia kopo moja bei yake ni elfu 65000. Bahati alisema msaada huo ni mkubwa ambao wamewapatia kwa ajili ya vifaa vitakavyotumika kufanya upasuaji wa koo,pua na masikio kwa wananchi watakaofika kupata huduma ya matibabu hayo