March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kivule yaongoza watiania nafasi ya Ubunge kuchukua fomu

Na Agnes Alcardo, Timesmajira

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, kimetoa takwimu ya watia nia wa nafasi ya Ubunge katika majimbo manne ya Wilaya hiyo hadi Juni 30, 2025 kufikia 49 huku kwa nafasi ya Udiwani wakiwa 194 kutoka katika Kata 36 zilizopo wilayani humo.

Kati ya majimbo hayo ni pamoja na Jimbo la Ilala, Segerea, Ukonga na Jimbo jipya la Kivule likionekana kuongoza kwa idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza kuchukua fomu ambao wamefikia 29.

Akizungumza na Waandishi wa Habari,Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Chief. Silvester Laredi, amesema hadi sasa bado watu wameendelea kuhamasika kujitokeza kuchukua fomu katika nafasi mbalimbali za kuwania uongozi.

” Wilaya ya Ilala hadi sasa tunaendelea vizuri na zoezi la watia nia kuendelea kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali,hadi leo takwimu zinaonesha Jimbo jipya la Kivule kuongoza kwa kuwa na idadi ya watia nia wengi,”amesema Yaredi.

Miongoni mwa watia nia waliojitokeza ni pamoja na mfanyabiasara maarufu jijini Dar-es-Salaam, Tickey Kitundu, ambaye amejitokeza kuchukua fomu ya kugombea Jimbo jipya la Kivule.

Tickey amesema, ana imani na chama hicho endapo kitampa ridhaa yapo mengi ambayo atayafanya katika Jimbo hilo.