January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiungo bora namba sita hucheza namba nne bila ya taabu

Na Philemon Muhanuzi, TimesMajira Online

NENO la kingereza ‘Holding Midfielders’, linamaanisha kiungo mkabaji mwenye jukumu la kusimama mbele ya mabeki wawili.

Pia lipo neno jingine la kingereza ‘Register’, lenye maana hiyo hiyo ya kiungo wa ulinzi ambaye pia anaitwa kiungo wa chini. Mara nyingi viungo wa chini huwa wanafanya kazi isiyosifiwa sana na mashabiki.

Hawana hulka ya kiuchezaji ya kuuremba mpira, hupewa kazi ya kuzunguka katika eneo lote la mbele ya mabeki wawili wa kati na wale wawili wa kulia na kushoto. Kwa sasa wapo viungo wakabaji wengi tu wenye soko.

Yupo Declan Rice wa West Ham, huyu ni kiungo mkabaji anayeweza kucheza kwa kiwango cha juu hata katika zile mechi ambazo timu yake inapambana na vilabu vikubwa vya Uingereza anao uwezo pasipo shaka wa kucheza namna sita na namba nne.

Yupo Wilfred Ndidi ambaye alinunuliwa na Leicester City kutoka klabu moja ya Ubelgiji. Waingereza hawajaijutia pesa waliyoitumia kumnunua. Ndidi ni chuma haswa cha Kinigeria, anazuia mashambulizi ya kila aina licha ya wembamba wake.

Na msimu huu makocha wa Leicester City wanamchezesha namba nne, mahali ambapo hajaonyesha kama vile anacheza kwa mara ya kwanza. Idrisa Gana Gueye ni kiungo wa zamani wa Everton ambaye kwa sasa anachezea PSG ya Ufaransa.

Gueye ni kiungo imara sana wa chini, mwenye uwezo wa kucheza namba nne. Yupo Mghana Thomas Partey, kwa haraka haraka ukimtazama utamuona akicheza soka la taratibu lakini kazi anayoifanya ni nzito sana.

Diego Simeone kocha wa Atletico Madrid anasifika kwa namna anavyoweza kupanga timu kwa nidhamu ya hali ya juu ya ulinzi, silaha yake muhimu amekuwa ni Partey.

Arsenal wanahangaika kuuza baadhi ya wachezaji ili wapate pesa ya kumnunua. Partey anacheza kwa uhuru kabisa nafasi ya beki namba nne iwapo makocha watamtaka acheze eneo hilo.

Fabinho wa Liverpool ni kiungo wa chini mwenye sifa ya ufungaji pale anapopata nafasi ya kupiga mashuti ya mbali. Fabinho amejaa yale maarifa ya kibrazil ya upigaji wa pasi zenye macho.

Sifa nyingine ni uwezo wa kucheza nafasi ya beki namba nne, kipindi hiki ambacho timu ina majeruhi wa ulinzi Fabinho anaifanya kazi ya kucheza namba nne akitumia akili nyingi katika upokonyaji wa mipira.

Casemiro haongelewi sana pale Real Madrid lakini ni mmoja wa wachezaji muhimu walioiwezesha timu kuchukua ubingwa wa ligi ya mabingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo.

Ana nguvu, anao uwezo wa kupokonya mipira na kucheza zile rafu za kadi ya njano wakati timu inapokutana na shambulizi la kushtukiza, anao uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya beki namba nne licha ya ukweli kwamba mabeki wa kati wa Real Madrid hawajakumbana na majeruhi kwa kipindi kirefu.

Ngolo Kante ni kiungo wa chini mfupi lakini udogo wa mwili alionao unafidiwa vyema sana na wepesi wake wa maamuzi.

Kwa wale wapenda soka wenye umri mkubwa Kante anawakumbusha namna Nico Njohole alivyokuwa enzi zile akiichezea Simba.

Kante anao uwezo wa kucheza nafasi ya beki namba nne ingawa ufupi wake huwa unawaogopesha makocha wanaoona ni bora abakie pale pale kwenye nafasi ya kiungo wa chini.

Granit Xhaka ni kiungo wa Arsenal mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya kiungo wa chini licha ya uwezo wake wa kupiga pasi zenye macho anapokuwa amesogea kushambulia.

Xhaka ameshatumika mara kadhaa kama beki namba nne kipindi Arsenal ikiwa na majeruhi wengi. Inter Milan imesumbua sana msimu uliopita na kama sio ubora wa Sevilla basi ilikuwa inabeba kombe la UEFA ndogo.

Yupo kiungo wa chini Marcelo Brozovic mwenye uwezo mkubwa kukaba na kuifanya kazi ya kina Romelu Lukaku kule mbele iwe ni nyepesi.

Brozovic anao uwezo wa kucheza kama beki namba nne bila ya wasiwasi wowote. Yupo pia Joshua Kimmich kiungo wa chini mwenye unyumbulifu wa kucheza maeneo mengi ya ulinzi.

Barcelona walipokea kipigo cha mbwa mwizi kutoka kwa Bayern Munich, huku wakishindwa kabisa kuwasumbua mabeki kwani Kimmich aliwanyima kibali.

Wapo viungo wengi wakabaji wanaotamba kwa sasa lakini wote wanayo sifa moja yenye kufanana, uwezo wao wa kucheza namba nne au ikibidi namba tano kutokana na mazingira ya mechi yalivyo.

Nikiwatazama viungo hawa wakabaji wanaotamba kwa sasa najikuta nikimkumbuka marehemu Method Mogella jinsi alivyokuwa na uwezo mkubwa wa kucheza namba sita, namba nne na namba nane bila ya wasiwasi wowote.

Pia najikuta namkumbuka Marehemu Issa Athumani namna alivyozimudu namba nyingi uwanjani zikiwemo namba sita, nne na kumi. Viungo wakabaji ni sehemu ya chachandu inayonogesha burudani ya soka.

%%%%%%%%%%%%%%