January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kituo cha umeme Kigamboni chakamilika

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online, Dar

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), Aprili 30, 2021 majira ya saa 4:28 usiku limefanikiwa kuwasha kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Dege Kigamboni.

Ujenzi wa kituo cha kupokea umeme cha Dege umefanywa na Wataalamu wa TANESCO, vifaa na mitambo vimeletwa na Mkandarasi Ms Telenergy d.o.o na njia ya umeme imejengwa na Mkandarasi Kampuni ya JV Tontan Ltd Group Six.

Kuwashwa kwa kituo hicho cha Dege kumeenda sambamba na uwashaji wa umeme kwenye njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka kituo cha Mbagala hadi cha Dege.

Kituo cha Dege kinatarajiwa kuwa mkombozi wa changamoto za umeme kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani.

Awali wananchi wa Kigamboni walipata umeme kupitia njia ndogo ya msongo wa kilovoti 33kV kutokea kituo cha Ilala na walikuwa wakikabiliwa na tatizo la umeme kukatika mara kwa mara pamoja na umeme kuwa mdogo.

Baada ya kuwasha kituo hicho umeme wa uhakika utapatikana katika maeneo yote ya wilaya Kigamboni ikiwemo maeneo ya Kimbiji, Mwongozo, Mwasonga, Pemba mnazi, Kisarawe2, na maeneo ya Viwanda vikubwa Wilayani hapo.

Mradi wa Dege ulianza kutekelezwa Mwezi Mei, 2019 kwa gharama ya shilingi 26.2 Bilioni.