Na Penina Malundo, timesmajira
ASILIMIA kubwa ya wananchi waishio vijijini wamekuwa wakitumia muda mrefu kufata huduma za afya katika vituo mbalimbali vya afya,zahanati na hospitali hali inayowafanya wengi wao kuishia njiani kwa kupoteza maisha huku wanawake kujifungulia njiani.
Hali hii imekuwa ikiwakumba wananchi wengi waishio Nyakahanga kata ya Rusumo kijiji cha Rusumo kukaa muda mrefu bila kuwepo kwa zahanati katika eneo lao na kutumia zahanati ya kijiji kingine ambacho kipo umbali wa Kilomita tano kukifikia.
Vestina Petro (25),mkazi wa Rusumo Boda anasema miaka mitatu ya nyuma walikuwa wakipata usumbufu sana wanapokuwa wanaugua hasa nyakati za usiku.
Anasema awali kituo cha afya kikubwa kilikuwa ni cha Mshikamano ambapo kipo kilometa tano kutoka rusumo boda hadi kufikia kijiji hicho hali ambayo ilikuwa inawagharimu muda na fedha nyingi wanapofata matibabu.
“Kabla ya kituo hiki kujengwa tuliangaika sana,sisi wakazi wa Rusumo kwani tulikuwa tukitoka hapa hadi Ngara kupata matibabu na ilikuwa ni changamoto sana kwetu,’’anasema na kuongeza
“Tulikuwa tukitumia gharama kubwa hasa kwa sisi wanawake ambao tunaenda kujifungua,unakuta uchungu unakupata usiku muda huo kivuko hakipo maana uwa mwisho saa 12 kufanya kazi yake hivyo inatugharimu kukodi gari ambapo gharama yake ni 50,000 kutoka hapa kwenda huko Ngara,’’anasema.
Anasema ukisema upande pikipiki hauwezi kupanda kwa sababu kuna umbali mrefu ila kwa mtu mgonjwa mwingine tofauti na Mama mjamzito anaepanda pikipiki ulipia kiasi cha sh. 20,000.
Petro anasimulia kuwa endapo umeugua ghafla na unataka kwenda Ngara katika kituo hicho cha afya ambacho ni kikubwa na hauna fedha madereva wa gari au pikipiki ukukopesha na kukupeleka hospitali.
“Kwa kweli sisi wakazi wa boda ya Rusumo tunashukuru sana huu mradi wa umeme wa maji wa maporomoko ya Rusumo yamekuwa na faida kubwa kwetu na familia zetu kwa kutujengea kituo cha afya ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwetu kwa sasa tunatembea muda mfupi sana na kutumia sh.2000 kufika hapa ,’’anasema na kuongeza
‘’Hii imekuwa rahisi kwetu tunapata huduma ya afya katika kituo hiki cha Rusumo,tunamshukuru Mungu sana,’’anasema.
Saraphina Gideoni (50) Mkazi wa Kijiji cha Mshikamano Rusumo anasema mwanzo walipata shida kabda ya kujengewa kituo cha afya cha Rusumo ambapo wananchi wa Rusumo wakienda zahanati ya Mshikamano.
Anasema katika zahanati hiyo ilikuwa inatoa huduma ndogo ndogo tu katika kupima maralia na magonjwa mengine lakini kwa magonjwa makubwa na upasuaji kama kujifungua walikuwa wanaenda Hospitali ya Wilayani Ngara.
‘’Kwa sababu ni zahanati hivyo tulipokuwa na matatizo makubwa kama kujifungua tulikuwa tunaenda huko Murugwanza na Nyamihaga zilizopo Wilayani Ngara hivyo kwa wanaoishi rusumo miundombinu inakuwa sio rafiki sana kwenda huko na kulazimika kuzunguka njia ya Benako hadi Ngara,’’anasema na kuongeza
‘’Tunashukuru sana kwa Kituo hiki cha Afya kimekuwa kinatupatia msaada mkubwa kwa sasa kwani tunapata matibabu kwa urahisi zaidi kwani tunapata vipimo karibia vyote ikiwemo UTI,Maralia na upasuaji mdogo.,’’anasisitiza.
***Daktari anazungumziaje huduma za afya Rusumo
Dkt. Josephat Zongwe Mganga Mfawidhi Msaidizi Kituo cha Afya Cha Rusumo,anasema kituo cha Afya cha Rusumo kinafanya shughuli mbalimbali za huduma kwa wagonjwa wa nje(Application Client) na wagonjwa wa ndani yaani wakulazwa.
‘’Pia kituo hiki kinatoa vipimo mbalimbali ikiwemo vya maabara kwa wagonjwa,huduma ya Kliniki ya Baba,Mama na Mtoto na wakinamama wajawazito wanajifungulia wanaohitaji upasuaji nao wanajifungua hapo,’’anasema.
Dkt. Zongwe anasema kufunguliwa kwa kituo hiki kimesaidia kupunguza wagonjwa wengi waliokuwa wanaenda hospitali ya wilaya ya Ngara kutokana na kufata matibabu makubwa.
‘’Watu wengi wanaofika katika hospitali yetu ni watu wanaotoka Kata ya Rusumo ambapo inavijiji vitatu ikiwemo Rusumo,Mshikamano na Kasharazi pia wanapokea wagonjwa wa kata nyingine za jirani kama Kasuru wote wanapata huduma za afya katika kituo hiki,’’anasema.
Aidha anasema sasa hivi hospitali hiyo inapokea wagonjwa wa maralia,wajawazito,mfumo wa upumuaji ikiwemo limonia ni kwa wingi ambapo walianza na wagonjwa 200 hadi 300 na sasa wagonjwa wanaoripoti katika kituo hicho wanafika 700 hadi 800 kwa mwezi kati yao wagonjwa 200 hadi 250 wanalazwa.
Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Rusumo,Atwemela Adolph anasema wanaishukuru Serikali pamoja na Wakala wa Mpango wa Bonde la mto Nile (Nile Basin Initiative NELSAP) kwa kujenga hospitali na kusogeza huduma kwa wananchi.
Anasema wananchi wa Rusumo walikuwa wanapata shida ya kupata matibabu kutokana na umbali ambao waliokuwa wanaenda kupata maribabu.
‘’Kwa sasa wananchi wamekuwa na furaha ya kupata neema na kushukuru kwa NELSAP kwa hatua waliyoifanya kwa ujenzi wa kituo hicho kwani tunashukuru vifaa vinapatikana na tunaamini changamoto mbalimbali zitaweza kutatulika kwa asilimia 100,’’anasema.
Anaseme mwanzoni hali ilikuwa mbaya kwani kulikuwa na kituo cha afya cha zahanati moja tu ya Mshikamano ambacho kilikuwa hakiwezi kutibu magonjwa mengi kwa huduma za Kihospitali kama upasuaji ambapo iliwagharimu wananchi kwenda Wilayani Ngara.
‘’Wananchi walikuwa wanaenda wilayani ngara kupata huduma na ukizingatia ni mbali sanaa pia gharama za usafiri zilikuwa ni kubwa hadi kufika huko hivyo changamoto kubwa ilikuwa mtu anapopata tatizo mida ya usiku kutokana na kivuko kufungwa mida ya jioni,’’anasema.
*** Mratibu wa Miradi ya Mendeleo ya Kijamii anazungumziaje ujenzi wa hospitali hiyo.
Mratibu wa Miradi ya Mendeleo ya Kijamii (LADP)inayosimamiwa na NELSAP,Irene Chalamira anasema Kituo hicho cha afya cha Rusumo kimegharimu kiasi cha Sh.Bilioni 1.5 kwa majengo 13 ikiwemo jengo la Wagonjwa wa Nje (ODP),maabara,mionzi,wamama kujifungua, kliniki ya baba,mama na mtoto ,jengo la kulazwa la magonjwa ,sehemu ya kufulia nguo,jengo la kuhifadhi maiti pamoja na nyumba tatu za watumishi wa kituo hicho.
Anasema kituo hicho kilianza kazi Februari,2022 lengo ikiwa ni kusogeza kituo cha afya kwa wananchi badala ya kutumia muda mrefu kutembea kufata huduma ya afya kwa vijiji vingine.
Chalamira anasema kabla ya NELSAP kujenga kituo hicho cha afya wananchi walikuwa wakitembea kwa umbali wa kilomita nne hadi tano kufata huduma za kiafya wilayani Ngara.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia