December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kisongo kuwekeza program ya makuzi na malezi

Na Queen Lema ,Timesmajira Online,Arusha

Taaasisi ya mafunzo Kisongo,(kisongo training institute)imefanikiwa kuanzisha programu maalumu ya malezi na makuzi ya watoto kwa kuwa taifa la baadae linategemea zaidi watoto.

Akiongea na waandishi wa habari Mkuu wa taaasisi hiyo Remy Julius amesema kuwa kwa sasa ni muhimu sana kwa walezi kupata mafunzo maalumu ya kuwalea watoto kwani kuna ongezeko kubwa la vituo ambavyo vinalea watoto.

Amesema kuwa ili watoto hao ambao wanalelewa katika vituo hivyo wakue vyema ni muhimu kwa walezi kuhakikisha wanakuwa na elimu hasa ya malezi.

“Malezi ni kitu muhimu sana ambacho kamwe hakipaswi kupuuzwa au kukiukwa na badala yake kinatakiwa kufanywa kwa weledi mkubwa ili kujua watoto wanataka ni nini ni lazina kuwa na maarifa ambayo yanatolewa,”.

Katika hatua nyingine amesema kuwa hata kwa vituo ambavyo vina husika na uleaji wa watoto ambavyo vimepata mafunzo ambayo yanatolewa na taasisi hiyo vimekuwa na utofauti mkubwa sana kwa kuwa suala zima la malezi ambayo yanaitajika kwa watoto yanatekelezwa tofauti na awali.

Pia amesema kuwa programu hiyo imeweza kusajili walezi zaidi ya 23 ambao wameweza kuwa mabalozi wazuri hasa katika malezi na makuzi ya watoto.

Huku akiwataka walezi hata wa vituo vya watoto kuhakikisha kuwa wanajiunga na programu hiyo ambayo ni muhimu kwa ustawi wa taifa la kesho.

Aidha amesema kuwa taasisi hiyo bado inaendelea kubuni programu mbalimbali ambazo zitakuwa na manufaa kwa jamii hasa kwa wahitimu ambao wanatarajia kujiajiri hasa katika sekta binafsi.