June 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kisa Oktoba 18, kigogo GSM awatega wachezaji Yanga

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BAADA ya ushindi mnono na wa kwanza kuupata msimu huu wa goli 3-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga, wadhamini wa klabu ya Yanga, Kampuni ya GSM ni kama wamewatenga wachezaji baada ya kuwaahidi ‘mkwanja’ mrefu endapo watafanikiwa kuwafunga wapinzania wao Simba katika mchezo wao wa Oktoba 18.

Ahadi hiyo huenda ikawapa morali zaidi nyota wa klabu hiyo kwani pia ni nafasi yao ya kulipa kisasi baada ya kukubali kichapo cha goli 4-1 zilizowafanya kutolewa katika hatua ya Nusu Fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup).

Yanga pia itaenda katika mchezo huo ikiwa na kocha mpya baada ya juzi usiku kutangaza kufikia makubaliano ya kusikitisha mkataba na kocha wao Zlatko Krmpotic ambaye amedumu ndani ya kikosi hicho kwa siku 37.

Kutimuliwa kwa kocha huyo ambaye aliahidi ndani ya mwezi mmoja atakuwa amesuka kikosi chenye nidhamu na ushindani wa hali ya juu ambacho kitaweza kuchukua alama tatu katika kila mchezo ni mwendelezo wake wa kutodumu katika klabu kwani katika baadhi ya timu ambazo amefundia
baada ya kukaa kwa siku 113 na Polokwane ya Afrika Kusini, amedumu simu 159 na APR lakini pia amekinoa kikosi cha Jwaneng Galaxy kwa siku 189.

Baadhi ya sababu zinazotajwa kumuondoa kocha huyo ni shinikizo kitoka kwa wachezaji ambao wameonekana kutoridhishwa ufundishaji wake jambo ambalo lilikuwa likiwapa wasiwasi huenda wakapoteza mchezo wao dhidi ya Simba.

Hata kabla ya mchezo dhidi ya Coastal kocha huyo alishajua kuwa huo ulikuwa mchezo wake ndani ya Yanga kwani inasemekana tayari alishawekwa kikao na Mshauri wa klabu hiyo Senzo Mbatha lakini pia tayari tetesi zilizanza kusikika kupitia mitandao mbalimbali toka baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo walianza kushikiza atimuliwe kutokana na mwendelezo wa ushindi wa goli moja katika mechi zao nne za kwanza.

Akizungumza baada ya ushindi dhidi ya Coastal, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said amesema kuwa, tayari wameshaandaa fungu nono kuelekea kwenye mchezo huo.

Amesema, toka msimu huu umeanza wameendelea na utaratibu wao wa kutoa bonas katika kila mchezo wanaoshinda lakini watakalopewa kuelekea mchezo huo huenda ikawa ni zaidi hata ya lile walilotoa msimu uliopita.

“Tayari tumeshatoa bonasi kwa michezo mitatu iliyopita na bonasi ya mchezo dhidi ya Coastal tutawakabidhi leo, lakini tunajipanga kutoa bonasi kubwa zaidi endapo wachezaji wetu watakafikiwa kushinda mchezo wetu wa Oktoba 18, ” amesema Injinia Hersi.

Amesema kuwa, kuelekea katika mchezo huo, jambo kubwa ni mashabiki mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuwapa morali wachezaji wao kwani mechi hiyo ni yao na dhamira yao ni msimu huu kutwaa ubingwa.

Lakini kabla ya kufutwa kazi, Zlatko amesema kuwa, ushindi waliopata Yanga katika mchezo dhidi ya Coastal Union haimaanishi kuwa wachezaji wapo vizuri kwani bado kuna mambo mengi hayapo sawa na ndio maana dakika za 45 za kipindi cha kwanza hakukuwa na muunganiko mzuri.

Amesema, kipindi cha pili wachezaji walijitahidi kubadilika na kupata goli tatu lakini hado hawakucheza vizuri kwani walianza kucheza kwa kuridhika na kuanza kucheza na jukwaa.

“Bado tuna kazi ya wachezaji wanatakiwa kufanya kazi ya ziada na kucheza vizuri na si kucheza na jukwaa kwani bado tuna mechi ngumu mbele yetu, ” amesema kocha huyo.