Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
WAFANYABIASHARA zaidi ya 50 wanadai kutishiwa kuondolewa kwenye majengo ya wakfu wanayofanyia biashara kutokana na deni la kodi ya pango,ambayo wamedai walilipa kwa kamati ya mpito ya Msikiti wa Ijumaa Jijini Mwanza.
Wakizungumza na waandishi wa habari, Februari 25,2025,wafanyabiashara hao wamesema wanakabiliwa na changamoto ya kufukuzwa kutokana na kudaiwa kodi ya pango,tayari baadhi wamepewa ilani (notice) ya kuondoka.Hivyo wameiomba Serikali iwasaidie wasiondolewe katika nyumba za wakfu wanazofanyia biashara.

“Viongozi wa Kamati ya Mpito walitutaka kulipa fedha za kodi mkononi mwao wakidai akaunti za msikiti zimefungwa, wana shida ya kulipa mishahara na huduma zingine.Awamu ya pili walikuja na hoja hiyo hiyo wakiongozana na madalali,wakatishia atakayekaidi kulipa watamwondoa,”amesema Abass Omary.
Ali Mukoko,amesema ni muathirika wa jambo hilo,baada ya kulipa benki milioni 10 za kodi ya miaka miwili (2024 na 2025), alifungiwa biashara kwa miezi sita na kufunguliwa kesi mahakamani.Hata hivyo hakupewa stakabadhi wala mkataba wa upangaji na sasa anadaiwa kodi ya miaka miwili ya nyuma iliyolipwa kwa kamati ya mpito kwa fedha mkononi.
“Wapo wapangaji wanadaiwa hadi milioni 42.Bodi mpya haitambui malipo yaliyofanywa mkononi na fedha haikuingizwa benki,hivyo tunaiomba Serikali itusaidie maana tuliowalipa fedha hizo wapo na wanafahamika kwa majina,”amesema.
Aidha,Wilfred Were,amesema wafanyabishara hawana ugomvi,kwa sababu fedha za pango wanazodaiwa waliilipa kamati ya mpito na kupewa stakabadhi, hivyo wanaomba warudishwe waendelee kufanya biashara ili kulinda mitaji yao,kwani baadhi wamekopa benki.
“Kamati ya mpito ya Msikiti wa Ijumaa inatajwa kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za msikiti huo,wafanyabiashara tulilipa fedha mikononi badala ya kupitia mifumo benki,bodi haitambui madeni tuliyolipa mkononi na kamati ya mpito haionekani,tunashindwa tuwapate wapi.Kwa vile suala hili liko TAKUKURU watusaidie ili tujue hatima yetu,”amesema Mandela Andrew.

Naye Shujaa Abdallah, amesema kamati ya mpito ilikuja na utaratibu wake na hawakuwa na uwezo wa kupinga,ndiyo sababu walilazimika kulipa fedha mkononi badala ya benki na kuiomba iwasaidie wapate haki yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Adhamini wa Msikiti wa Ijumaa, Abdallah Amin Abdallah ,akizungumzia kadhia hiyo amesema baada ya bodi yao kuvunjwa mwaka 2019, ikaundwa kamati ya mpito na kutambulishwa kwa wapangaji wakaelekezwa wasilipe fedha mkononi.
Amesema kuwa waliwashauri wapangaji hao wawatafute waliowapa fedha mkononi ama wazipeleke wenyewe (kamati ya mpito) benki, watuletee slip tuwape stakabadhi waendelee kufanya biashara.
“Sisi hatuna ugomvi nao tunasimamia maagizo ya Serikali,Kabidhi Wasii Mkuu,aliagiza wakalipe kielektroniki.Wakachukue hatua ya kuwatafuta na kuwafungulia mashitaka waliowakabidhi fedha.Kama sikosei suala hili liko TAKUKURU,tutawaondoa na huo ndio msimamo wa bodi,”amesema Abdallah.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Kanyusi, amekiri kwa simu kuwa kamati aliyoiunda ilibaini ubadhirifu wa fedha za Msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza na kupeleka suala hilo kwa mamlaka za uchunguzi.
“Baada ya uchunguzi wa kamati nilikabidhi suala hilo kwa vyombo vyenye mamlaka ya uchunguzi na kuwafikisha wahusika mahakamani kwa sababu walitenda jinai.Kwa vile liko kwenye uchunguzi nimefungwa mikono na sina tena mamlaka,wanaoweza kulizungumzia liko hatua gani na kuwafikisha mahakamani ni TAKUKURU Mwanza,”amesema.

More Stories
Watafiti wa mimea vamizi watua Serengeti
Meya akabidhi Televisheni na king’amuzi Yanga
Mwenyekiti ALAT afanya dua kumshukuru Mungu kwa uhai