Na Mwandishi wetu,Timesmajira
WITO umetolewa kwa watu binafsi na waandaaji wa matukio wanaotaka kuendesha mashindano rasmi ya Miss World Tanzania kwa ngazi ya mkoa kuwasilisha maombi yao ili waweze kupata leseni ili waweze kuendesha mashindano hayo katika maeneo yao husika.
Wito huo umetolewa leo jijinj Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kitaifa wa Miss World Tanzania, Mustafa Hassanali wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa hilo lililochini ya Kampuni ya 361 Degrees Africa linalolenga kuwatambua, kulea na kuwawezesha wasichana wa Kitanzania ili kuwakilisha taifa kwa heshima, urembo, akili na dhamira.
Amesema wamiliki wa leseni watakaoidhinishwa watapewa mamlaka ya kipekee kusimamia mashindano hayo katika mikoa yao ili kuhakikisha ushiriki unakuwa mpana kwa nchi nzima.

“Mashindano ya ngazi ya mikoa yatafanyika kupitia wamiliki wa leseni watakaorasimishwa nchini kote. Matukio haya yatachagua washiriki bora watakaopanda hatua hadi fainali za kitaifa jijini Dar es Salaam, hivyo kuhakikisha ujumuishwaji na fursa sawa kwa wasichana kutoka kila mkoa,” amesema Hassanali.
Amesema kupitia Jukwaa hili litaanzisha enzi mpya ya urembo wenye malengo katika kuwatambua na kuwalea wanawake vijana wenye uwezo wa kipekee wanaoonyesha umahiri, uongozi na falsafa ya kimataifa.

“Dhamira yetu ni kutoa jukwaa linalokuza sauti zao, kuimarisha jamii zao na kuwaandaa kuiwakilisha Tanzania kwa fahari na ubora katika jukwaa la kimataifa la Miss World,” amesema

Aidha amesema Mshindi wa shindano la kitaifa atabeba taji la Miss World Tanzania na kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mashindano ya Miss World 2026 kama balozi wa urembo, utamaduni na dhamira ya ubinadamu.Katika hatua nyingine Hassanali amewahimiza wazazi na walezi kuwaunga mkono watoto wao wa kike ili waweze kushiriki katika jukwaa hilo ambalo amesema lina uwezo wa kuinua na kubadilisha maisha yao.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako