December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kipaumbele cha Rais Dkt. Samia sekta ya afya na mafanikio yake

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

KWA kutambua umuhimu wa kuwa na afya bora kwa wananchi wote, Rais Samia Suluhu Hassan, ameendea kufanya jitihada mbalimbali ili kupambana na adui maradhi.

Rais Samia amekuwa akifanya hivyo akitambua kuwa maradhi ni miongoni mwa maadui wakubwa wa maendeleo nchini.

Ndiyo maana Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia imeendelea kutoa kipaumbele kwa Sekta ya Afya, ambapo katika Mwaka 2021/22, Serikali ilitenga sh. Trilioni 2.1, Mwaka 2022/23 ilitenga Trilioni 2.2 na Mwaka 2023/24 imetenga Trilioni 2.4. kwa ajili ya sekta hiyo.

Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika uwekezaji huu ni pamoja na;
Miundombinu ya Utoaji wa Huduma za Afya Wizara. Aidha, Rais Samia ameendelea kusimamia upatikanaji wa huduma za afya nchini zinazotolewa kupitia Vituo vya kutolea huduma vya Serikali, binafsi na mashirika ya Dini.

Akithibitisha hilo, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Dkt. Godwin Mollel, anasema katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Machi, 2023, vituo vya kutolea huduma za afya nchini vimeongezeka kufikia jumla ya vituo 11,040 ikilinganishwa na vituo 8,549 mwaka 2021.

Kati ya hivyo, Hospitali zilikuwa 430, vituo vya afya vilikuwa 1,030, Zahanati zilikuwa 7,458, Kliniki zilikuwa 906 na Maabara Binafsi 1,216.

Anasema juhudi hizo za Rais Samia zinawezesha sehemu kubwa ya wananchi kupata huduma za afya karibu na maeneo wanayoishi hivyo kuwapunguzia gharama wananchi.

“Serikali imeendelea kukamilisha ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa katika mikoa mipya ya Njombe, Songwe, Geita, Simiyu na Katavi. Awamu ya kwanza ya ujenzi huo imekamilika na tayari hospitali zote zimeanza kutoa huduma. Aidha, Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Kusini Mtwara na Hospitali ya Kanda Chato ambapo tayari huduma zimeanza kutolewa,” anasema Dkt. Mollel.

Vilevile, anasema Serikali imeimarisha miundombinu ya kutolea huduma za Dharura nchini kwa kujenga majengo ya huduma za dharura (EMD) 128 katika Hospitali ngazi ya Taifa, Maalum, Kanda na Mkoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba hadi Machi mwaka 2023 na ICU 73 zimejengwa na kukamilika hadi kufikia Machi 2023.

Anafafanua kwamba kuimarika kwa huduma hizi kumewezesha hospitali kuokoa maisha ya wagonjwa ambao wanauhitaji wa huduma hizo kwa asilimia 20 hadi 40.

Kwa mujibu wa Dkt. Mollel uwekezaji huu katika miradi ya maendeleo umegharimu zaidi ya sh. Billioni 891.5

Anasema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika eneo la huduma za uchunguzi ambapo Jumla ya Mashine za MRI 7, CT-Scan 32, Digital X-ray 199 na Angio-Suite 1 ambayo inawezesha kufanya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu zimenunuliwa. Uwekezaji huu umewezesha Nchi yetu kuwa na jumla ya MRI 13, CT-Scan 45 na Digital X-ray 543.

“Uwekezaji huu umewezesha upatikanaji wa huduma za uchunguzi karibu zaidi na wananchi ambapo hapo awali huduma za MRI na CT Scan zilikuwa zinapatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwalazimu wagonjwa kutumia gharama kubwa kufuata huduma hiyo. Vilevile uwekezaji huu umeimarisha huduma za tiba kwa kuwa Wataalam wanakuwa na uhakika na ugonjwa alionao mteja na kutoa tiba sahihi,” anasema Dkt. Mollel.

Anaongeza kwamba Serikali imeendelea kuwekeza katika upatikanaji wa dawa ambapo katika kipindi cha awamu ya 6, jumla ya sh. Bilioni 442 zimetolewa.

Aidha, kwa mwaka 2022/23 Serikali ilitoa zaidi ya asilimia 90 ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa (Bilioni 190). Uwekezaji huu umewezesha upatikanaji wa dawa nchini kuongezeka kutoka asilimia 37 mwaka 2021 hadi wasani wa asilimia 75 mwaka 2023 katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini
Kuimarisha Huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi.

“Serikali imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa hapa nchini kwa kuendelea kuweka utaratibu mzuri wa kusomesha watumishi ujulikanao kwa jina la Samia Health Super specialisation Program ambapo katika mwaka 2023/24 Serikali imeongeza fedha za udhamini wa masomo kufikia bilioni 9 kutoka bilioni 5 iliyokuwa imetengwa mwaka 2022/23. Kupitia Mpango huu, jumla ya wataalam wapya 300, wataalamu 848 wanaoendelea na masomo na wataalam 100 kwa utaratibu wa seti watagharamiwa masomo yao ndani na nje ya nchi,” Anasema.

Anasema Mfumo wa Ugharamiaji wa huduma za afya Tangu na baada ya uhuru wananchi wamekuwa wakipata huduma za matibabu bila malipo, ambapo Serikali imekuwa ikigharamia huduma hizo.

Hata hivyo, anasema kutokana na changamoto za kiuchumi katika miaka ya 90, Serikali ilianzisha mfumo wa kuchangia huduma za matibabu kupitia utaratibu wa malipo ya papo kwa papo, msamaha kwa makundi yasiyo na uwezo na malipo kabla ya kuugua yaani bima ya afya.

“Pamoja na juhudi hizo bado kumekuwa na changamoto ya wananchi kuchangia huduma za matibabu kupitia mfumo wa malipo ya papo kwa papo (fedha taslim) na utoaji wa huduma kupitia utaratibu wa msamaha,” anasema.

Kutokana na changamoto hizo, Serikali ilianzisha mfumo wa malipo kabla ya kuugua (Bima ya Afya) kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuanza na kundi la watumishi wa umma na wategemezi wao ambao hujiunga kwa mujibu wa Sheria Sura.

Hata hivyo, kutokana na uhitaji wa bima ya afya kwa makundi mengine ya wananchi, Serikali imekuwa ikifanya marekebisho ya Sheria ya bima ya afya ili kuruhusu makundi hayo kujiunga kwa hiari.

Anasema kwamba Takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia Juni 2023, wanufaika wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya walikuwa 4,821,233 sawa na asilimia 8 ya wananchi wote.

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya kupitia mfumo wa bima ya afya, bado kuna changamoto katika ujumuishwaji wa wanachi katika mfumo huo kutoka katika sekta rasmi binafsi na isiyo rasmi.

Anasema vhangamoto hiyo ni uhiari wa kujiunga kwa makundi hayo kwakuwa wengi hujiunga wakiwa tayari ni wagonjwa.

Mathalan, mwaka 2016 Mfuko ulianzisha mpango wa bima ya afya kwa watoto walio chini ya miaka 18 (Toto Afya Kadi) kwa lengo la kuwezesha kundi la watoto kwa ujumla wao kujiunga kupitia shule za awali, msingi na sekondari ili kunufaika na mpango huo.

Hata hivyo, pamoja na uhamasishaji uliofanyika kwa kupindi cha takriban miaka saba, bado mwitikio haukuwa wa kuridhisha kwani idadi ya watoto waliojiandikisha ilikuwa ni 210,000 kati ya lengo la watoto milioni 25 kwa kipindi hicho.

Aidha, kupitia uandikishaji wa kundi hilo, asilimia 99 ya watoto walioandikishwa walikuwa tayari na matatizo ya kiafya ambapo kati ya takriban sh. bilioni 5 zilizokusanywa kama michango yao, shilingi bilioni 40 zilitumika kugharamia matibabu yao.

Hali hii ni kinyume cha dhana na misingi ya uendeshaji wa mfumo wa bima ya afya.

Hivyo, ili mfumo wa bima ya afya uwe endelevu, ni lazima kila kundi linaloandikishwa liwe na uwezo wa kuchangiana gharama za matibabu.

Katika kutatua changamoto zilizopo, Serikali inakamilisha muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo inalenga kuimarisha Mfumo wa Bima ya Afya nchini kwa kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanajiunga zaidi na utaratibu huu ikilinganishwa na hali ilivyo sasa. Nitoe rai kwa wananchi wote ambao bado hawajajiunga na utaratibu wa bima, wajiunge sasa na pia pindi maamuzi yatakapofanyika, wajitokeze kwa wingi kujiunga na Mfumo huu.

Pamoja na jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya, kuongeza bajeti ya dawa na vitendanishi, kuwajengea uwezo watumishi wa sekta ya afya na kuongeza watumishi wa Sekta ya Afya, bado kuna changamoto ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya wananchi wenye magonjwa yasiyo ya kuambukizwa na gharama zake.

Anasema katika kipindi cha awamu zote sita, Serikali imefanikiwa kuboresha Sekta ya Afya kwa ujumla, changamoto kubwa iliyobaki na inawayolikabili kundi kubwa la wananchi ni namna ya kuwawezesha wananchi kugharamia huduma za afya.

Kwa hiyo, ili kufikia dhamira ya Serikali ya Afya Bora kwa Wote ni lazima kama nchi kuwa na mfumo endelevu na imara wa uchangiaji wa gharama za matibabu kabla ya kuugua (bima ya afya).

Hivyo, kupitia hadhara hii, nawaomba sana wanahabari na vyombo vya habari kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi na hasa mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Afya ili wananchi waelewe juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.