January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi wa Mwenge ataka taarifa za wenye walemavu

Na Esther Macha, Timesmajira,Online,Mtwara

KIONGOZI wa mbio za Mwenge Kitaifa, Luteni Josephine Mwambashi, ameagiza uongozi wa wilaya ya Mtwara Vijijini kuandaa taarifa ya watu wenye ulemavu ili ipelekwe kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kufanya uchambuzi na kuwatambua watu wenye mahitaji maalum.

Amesema hatua hiyo itawawezesha kutambua watu wenye ulemavu ambao hawana
vifaa saidizi.

Luteni Mwambashi amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kupokea taarifa ya watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Mtwara Vijijini wakati Mwenge wa Uhuru ulipofika wilayani hapa.

Kupitia mbio hizo za Mwenge ilizinduliwa miradi mbalimbali ikiwemo vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu ,shamba la michikichi ,pamoja na miradi mingine katika wilaya hiyo.

“Nimempa Mratibu wa Mkoa sampo ya wilaya nyingine tuliyotoka ili achukue sampo ile kwa ajili ya kuandaa taarifa ya walemavu iliyokamilika na kwenye risala ya utii itapokelewa ikiwa na taarifa ya walemavu ambayo itaenda moja kwa moja kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kufanya uchambuzi na kuwatambua watu wenye mahitaji maalum ili kwa wale ambao hawana vifaa na mambo mengine,” amesema.

Akisoma taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, mwanafunzi mlemavu wa shule ya sekondari Mustapha Sabodo, Said Hassan alisema halmashauri ya Wilaya Mtwara inatambua watu wenye ulemavu uwepo wao mahitaji yao na mchango katika shughuli za maendeleo watu wenye ulemavu waliotambuliwa katika halmashauri ya Mtwara ni 1,362 kati yao wanaume ni 615 na wanawake ni 747.

Aidha amesema kundi hilo maalum lina watoto 381 na watu wazima 981 na mchango wa taarifa ya hali ya ulemavu aina ya ulemavu wa viungo watu wazima, 482 na chini ya miaka 18 170 jumla 656 ,walemavu wa ngozi 61,

Hata hivyo, amesema halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kwa kutambua mahitaji muhimu ya walemavu imekuwa ikishirikiana na waau mbali mbali ili kuhakikisha vifaa mbali mbali vya watu wenye ulemavu vinapatikana .

Aidha, Mwambashi alizindua madarasa mawili ya shule ya msingi Msijute na ofisi ya walimu ambapo alisema kuwa wameridhishwa na kiwango cha ujenzi.

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mustapha Sabodo iliyopo Mtwara Vijijini wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Erica Yegella.

“Ndugu zangu wananchi naendelea kuwasisitiza tunapopewa dhamana ya kusimamia miradi lazima kuwashirikisha wananchi na fedha inapokuja wananchi wapewe taarifa ili wawe na uwezo wa kuridhia miradi yao, sababu miradi hii inahusu wananchi wote,”alisema kiongozi huyo wa mbio za Mwenge.

Akifafanua zaidi, Luteni Mwambashi amesema wamekagua utendaji wa Mhandisi wa mradi kuna nyaraka ambazo hakuwa amendaa ambazo zinaonesha matumizi yaliyotumika mpaka mradi ulipofikia wakilinganisha na kazi ,kupitia mradi huo wanapopewa dhamana ya kusimamia miradi wafanye kazi yao inavyotakiwa hasa nyaraka na mtu akija kwenye jengo kama hilo ambalo limekamilika na lipo vizuri kumdhihirishia lazima kupanga nyaraka vizuri na kuelezea vizuri pamoja na kuandaliwa kwa ukamilifu.