Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi amesema tangu ameingia Mkoa wa Tanga Juni 6, mwaka huu amekuwa akiridhika na ujenzi wa miradi ya maji na kummwagia sifa Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wa mkoa huo Mhandisi Upendo Lugongo kuwa anafanya kazi nzuri.
Akizungumza Juni 11, 2025 kabla ya kuweka Jiwe la Msingi kwenye Mradi wa Ukarabati wa Miundombinu ya Maji katika Mji wa Lushoto, Ussi alisema akiwa ameshatembelea halmashauri sita kati ya 11 za mkoa huo, miradi yote amekuta ni mizuri, lakini miradi ya maji ambayo ipo kwenye halmashauri zote alizotembelea, ina ubora zaidi.
“Kipekee, nikushukuru sana Meneja wetu wa RUWASA Mkoa wa Tanga (Mhandisi Upendo Lugongo). Kwa kweli dada yangu na Mama yangu tunakushukuru sana. Kwa kweli hapa tunaendelea kupata tafsiri kuwa wanawake wanaweza. Kwa kweli wewe umekuwa na speed (kasi) kubwa ya ufanyaji kazi, kwa kweli unaendelea kumuaminisha Rais Dkt. Samia (Suluhu Hassan) kuwa wanawake wakipewa nafasi yeyote ile wanaweza kuitendea haki kwa wananchi.

“Kama anavyoitendea yeye nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini na ninyi wasaidizi wake kwa kweli mnaendelea kumuwakilisha vizuri, tunakushukuru sana, tunakupongeza sana, pamoja na timu yako yote ambayo unayoiongoza katika eneo lako. Kwa kweli leo hii RUWASA ninapokuja kwenye miradi yenu kwa kweli sina shaka ya aina yeyote. Huwa nauliza, huu mradi unasimamiwa na nani, nikiambiwa tu na RUWASA wamo, huwa roho yangu imesharidhika sababu mnafanya kazi nzuri sana” amesema Ussi.
Ussi amesema kila anapotembelea miradi ya maji ameona wananchi wanavyofarijika kutokana na kuwepo miradi hiyo, hivyo amewataka wananchi kuwaunga mkono wanatendaji wa mamlaka za maji na Serikali kwa kuhakikisha miradi hiyo inalindwa na kuwa endelevu, kwani tenki la pili linalojengwa litaongeza upatikanaji wa maji kwenye Mji wa Lushoto, na wananchi wengi wataweza kuvuta maji ndani ya nyumba

Baada ya kutembelea miradi kadhaa ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, aliimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Dkt. Ikupa Mwasyoge, kuwa miradi yake ina viwango.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Lushoto (LUSHUWASA) Mhandisi Mdathiru Mtanda amesema ukarabati wa miundombinu ya maji Lushoto ni miongoni mwa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na LUSHUWASA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (HTM) kupitia fedha za Mfuko wa Maji. Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi SAXON BUILDING CONTRACTORS LIMITED wa DAR ES SALAAM kwa Mkataba Namba TR163/2023/2024/W/09 wenye thamani ya sh. 1,186,954,200.Â

“Utekelezaji wa mradi huu ulianza rasmi Aprili 16, 2024 na ulitegemea kukamilika Aprili 16, 2025. Hata hivyo, Mkandarasi ameongezewa muda wa siku tisini kutokana na kampuni ya Saxson kufiwa na Mkurugenzi Mtendaji, hivyo mradi utakamilika Julai 17, 2025. Mradi unatarajiwa kuhudumia wananchi 23,118. Maeneo yatakayohudumiwa na mradi huu ni Yoghoi, Magamba Kosti, Girrafe, Chakechake, Maguzoni, Mabwawani na Dochi.
“Mradi huu ukikamilika utaongeza uzalishaji wa lita 420,290 kwa siku na kazi zinazofanyika ni pamoja na:
ujenzi wa chanzo eneo la Kivumbi umefikia asilimia 20, ujenzi wa tenki la Maguzoni lita 90,000 asilimia 40,
ujenzi wa tenki Magamba lita za ujazo 50,000 asilimia 35, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba Kilomita 25.115 zimekamilika kwa asilimia 47, ununuzi wa vifaa na viungio (fittings) asilimia 45 na ujenzi wa tenki Yoghoi lita 90,000 asilimia 50″ amesema Mhandisi Mtanda.
Mhandisi Mtanda amesema, mradi huo unagharimu sh. 1,186,954,200 hadi kukamilika kwake, na mpaka sasa Mkandarasi amelipwa malipo ya awali (advance payment) sh. 178,043,130, na kwa sasa mradi umefikia asilimia 50. Mkandarasi yupo eneo la kazi anaendelea na kazi, aidha maeneo ya Mshuza na Kwelusase yameshaanza kuhudumiwa maji na mradi huo.

“Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Lushoto tunatoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha za miradi ya maendeleo, tutazisimamia vizuri ili ziweze kuleta tija kwa wananchi na kufikia malengo yaliyokusudiwa” amesema Mhandisi Mtanda.


More Stories
Teknolojia yawezesha wastaafu kupata huduma za PSSSF kwa urahisi
CP.Wakulyamba awataka maofisa wa NCAA kuwa wabunifu
Kipanga azindua kituo cha Mawasiliano,Serikali yaahidi elimu bora kwa Wote