December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi mbio za Mwenge kitaifa ampongeza Samia kwa mradi wa maji Bumbuli

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Bumbuli

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maji nchini.

Kwani ameona matokeo chanya wakati alipofika kwenye mradi wa maji Funta uliopo Halmashauri ya Bumbuli mkoani Tanga ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 4,782 wa vijiji viwili vya Funta na Manga, Kata ya Funta.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akikata utepe kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi mradi wa maji Funta,kulia ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo, na kushoto ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga

Ameyasema hayo Aprili 11, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi, ambapo ameeleza kuwa licha ya mradi kufikia asilimia 80 ya utekelezaji wake tayari baadhi ya wananchi wanapata maji.

“Rais ameleta fedha hapa kiasi cha milioni 800 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji ambao umefikia asilimia 80 ya utekelezaji, tumepata taarifa ya kwenye chanzo, kwenye tenki la maji na hata usambazaji wa maji, tenki hili ambalo lina ujazo wa lita 120,000, linakwenda kuwasaidia wananchi zaidi ya 4,000,”ameeleza Mnzava na kuongeza kuwa

“Tunapenda kumshukuru Rais Dkt. Samia na kumpa maua yake kwani anaendelea kuguswa na changamoto za wananchi na kwa utashi wake na utayari wa kuendelea kuleta huduma karibu,”.

Mnzava pia, amemshukuru Amina Shengovi wa Kijiji cha Funta aliyetoa eneo lake la kipande cha ardhi ili kujengwe tenki la mradi wa maji Funta kwani kitendo hicho ni cha kizalendo na katika kuonesha shukrani hizo, RUWASA Wilaya ya Lushoto wamemuwekea kituo cha kuchota maji (kilula) ambapo atachota maji bure kwa mwaka mmoja.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akiweka Jiwe la Msingi mradi wa maji Funta wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Jafar Kubecha (kushoto) na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lushoto Ali Daffa (katikati)

Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga amesema ujenzi wa miundombinu ya maji katika mradi wa Funta ni miongoni mwa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na ofisi ya Meneja wa RUWASA Lushoto kupitia fedha za Mfuko wa Maji.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi MS Koberg Construction Company Ltd ya mkoani Dar es Salaam kwa mkataba Namba AE-102/2021-2022/TAG/W/61 wenye thamani ya bilioni 2.7.

“Utekelezaji wa kazi kwa eneo la Funta ulianza rasmi Agosti 18, 2022 na unategemea kukamilika Aprili 30, 2024.huku kazi zinazofanyika ni pamoja na
ujenzi wa tenki la lita 120,000 ujenzi umefikia asilimia 90, uchimbaji wa mtaro mita 1,300 za Gravity main asilimia 95,
uchimbaji mtaro mita 9,527 za distribution lines asilimia 100,ulazaji wa bomba asilimia 95 na ujenzi wa vituo vya maji 23 asilimia 65 (vimejengwa 15),” ameeleza na kuongeza kuwa

“Mradi huu unagharimu jumla ya milioni 832.6, Mkandarasi yupo site anaendelea na kazi za ujenzi wa vituo vya maji pamoja na ulazaji bomba kwenye vituo hivyo,mpaka sasa Mkandarasi amelipwa kiasi cha milioni 264.9 kama malipo ya awali,”.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akimsikiliza Amina Shengovi ambaye alitoa eneo lake kujengwe tenki la maji
Timu ya RUWASA ikiongozwa na Meneja wa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (katikati) ikifurahia baada ya Mradi wa Maji Funta kuwekewa Jiwe la Msingi
Tenki jipya la Mradi wa Maji Funta (kulia), na tenki la zamani kushoto