Na Albano Midelo
SHULE ya sekondari ya Kigonsera iliyopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma ina historia ya kipekee hapa nchini kwa sababu ndiyo sekondari iliyoweza kuwatoa viongozi wawili wa ngazi ya juu kabisa nchini.
Ponsiano Ngungulu ni Mkuu wa sekondari ya Kigonsera anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1938 ikiwa ni seminari ya kanisa katoliki chini ya Shrika la Wabenedikitini(Benedictine fathers) wa Peramiho hadi mwaka 1961 ilipochukuliwa na serikali.
Ngungulu anasema shule hiyo ya wavulana pekee, ina uwezo wa kuwahudumia wanafunzi 280 na kwamba tangu kuanzishwa kwake hadi sasa,shule hiyo imeweza kutoa jumla ya wahitimu 13,266.
“Shule wakati inaanzishwa na wakoloni ilikuwa na lengo la kutoa elimu ya dini ya kikristo hususani dhehebu la kanisa katoliki hivyo baada ya uhuru serikali iliamua kuitaifish ili iweze kuwahudumia watanzania wote bila ubaguzi wa kidini’’,anasema.
Hata hivyo anasema tangu mwaka 1961 hadi mwaka 2011 sekondari ya Kigonsera imekuwa inatoa elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne na kuanzia mwaka 1998 hadi sasa sekondari hiyo imekuwa inatoa elimu ya kidato cha sita.
Sekondari ya Kigonsera imepata umaarufu mkubwa hapa nchini kwa sababu imeweka historia iliyotukuka baada ya viongozi maarufu wa kitaifa kusoma katika sekondari hiyo.
Mkuu wa sekondari ya Kigonsera anamtaja mmoja wa viongozi hao kuwa ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Benjamin Mkapa ambaye alisoma Kigonsera toka mwaka 1952 hadi 1953.
Ngungulu anamtaja Kiongozi mwingine wa kitaifa ambaye amesoma Kigonsera ni Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye alianza kidato cha kwanza na kuhitimu kidato cha nne katika sekondari hiyo mwaka 1980.
Licha ya viongozi hao sekondari ya Kigonsera imetoa viongozi wengine wengi hapa nchini ,miongoni mwao ni Dkt.Modestus Kipilimba ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji,Profesa Simon Mbilinyi aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Mbunge wa Peramiho na Juma Homera Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Viongozi wengine waliosoma Kigonsera ni Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt.Frolens Turuka,Hayati Askofu Mstaafu wa Jimbo la Mbinga Imanuel Mapunda,Hayati Askofu Mstaafu wa Jimbo la Njombe Raymund Mwanyika ,Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Songea Norbeth Mtega,Askofu wa Jimbo la Lindi Mhashamu Bruno Ngonyani ,Askofu wa Jimbo la Mtwara Mhashamu Gabriel Mmole na Askofu wa Jimbo la Njombe Mhashamu Alfred Maluma .
Mkuu wa shule anawataja walimu waliopo hivi sasa katika sekondari hiyo kuwa ni 37 na kwamba idadi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita kwa mwaka 2019/2020 wanafikia 776 kati yao 414 ni wa kidato cha tano na 362 ni wa kidato cha sita.
Shule ya sekondari ya kigonsera kwa miaka mitatu mfululizo imekuwa inafanya vizuri kitaaluma mwaka 2017 tulifaulisha kwa asilima 97,mwaka mwaka 2018 kwa asilimia 98 na mwaka 2019,tulifaulisha kwa asilimia 99.52’’,anasema Ngungulu.
Licha ya mafanikio yaliyopatikana Mkuu wa shule hiyo anazitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni ubovu wa barabara ya kuingilia shuleni ,uchakavu wa nyumba 18 za walimu na ukosefu wa watumishi wasiokuwa walimu hasa wapishi,dereva,karani na wahudumu wa ofisi ya Mganga.
Changamoto nyingine anazitaja kuwa ni upungufu wa walimu sita wa masomo ya Sayansi,uchakavu wa magari ya shule,ukosefu wa maktaba,zana hafifu za kilimo ili kuwafundisha wanafunzi kilimo cha kisasa kinachoendana na sera ya viwanda na upungufu wa fedha za kununulia vifaa vya Sayansi na kemikali.
Hata hivyo anasema katika kujiongezea mapato shule hiyo inafanya elimu ya kujitegemea ambapo shule inamiliki shamba la ekari 30 na katika msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019 wamefanikiwa kuvuna jumla ya tani 26 za mahindi na kwa kwamba shule pia ina mradi wa ng’ombe saba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akizungumza baada ya kutembelea shule hiyo anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa zaidi ya milioni 930 za kukarabati sekondari hiyo kongwe nchini ambayo majengo yake yalikuwa yamechakaa.
Mndeme anasema mazingira ya shule hiyo yamekuwa rafiki baada ya ukarabati mkubwa wa majengo mbalimbali ya shule na nyumba mbili za walimu ambapo hivi sasa muonekano wa shule hiyo unavutia.
Hata hivyo Mndeme amewaagiza TARURA wilaya ya Mbinga kukarabati barabara inayofika katika shule hiyo ili iweze kupitika wakati wote ikiwa ni sehemu ya kuwaenzi viongozi wa kitaifa ambao wamesoma katika shule hiyo .
“Lazima tuendelee kuitunza historia ya shule hii kwa kusomesha viongozi wa kitaifa Rais Mstaafu Mkapa na Waziri Mkuu Majaliwa wamesoma hapa,ni lazima changamoto zote zinazoikabili shule zitafutiwe ufumbuzi,shule hii ni urtihi wetu katika Mkoa wa Ruvuma’’,anasisitiza Mndeme.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika