Na Penina Malundo, Timesmajiraonline
ZIARA ya kitaifa ya Rais Samia Suluhu Hassan, nchini Cuba imeahirishwa kutokana na taarifa za kuchafuka kwa hali ya hewa kutokana na kimbunga cha Rafael.
Kimbunga hicho kilipiga visiwa vya Cuba na mji mkuu wa Havana.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisema Rais Samia alitarajiwa kuwasili nchini Cuba kuanzia Novemba 6 hadi 8, 2024, kwa ajili ya Kongamano la Kimataifa la Lugha ya Kiswahili.
Balozi Kombo alieleza kuwa kimbunga hicho kililipuka kwa masaa kadhaa, hali ambayo ilisababisha viwanja vyote vya ndege nchini Cuba kufungwa kwa takribani masaa 48, ikiwemo Kiwanja cha Ndege cha Jose Marti, kilichozunguka mji mkuu wa Havana.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, safari ya Rais Samia itafanyika katika tarehe zijazo, ambapo tarehe maalum itatangazwa rasmi.
Aidha, kuhusu Tamasha na Kongamano la Kimataifa la Lugha ya Kiswahili, Balozi Kombo alisema kuwa shughuli hizo zitaendelea kama ilivyopangwa, chini ya usimamizi wa Mawaziri waliokuwepo, wakiwemo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ndumbaro, ambaye atakuwa msimamizi mkuu wa kongamano hilo.
Vilevile, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Mwita, watakuwa sehemu ya kongamano hilo.
More Stories
Madiwani Korogwe TC wahakikishiwa maji ya uhakika
CHADEMA wampongeza Mkurugenzi Mpanda
Ukosefu wa maji wasababisha wanafunzi kujisaidia vichakani