December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kimbunga Jobo chayeyuka Tanzania, TMA yathibitisha

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Nchini (TMA),imesema kimbunga hafifu “Jobo”kilichotarajiwa kutokea Aprili 25,mwaka huu katika mikoa ya Pwani ikiwemo Dar es Salaam hakipo katika nchi ya Tanzania na hakuna madhara ya moja kwa moja yanayotarajiwa kutokea.

Taarifa iliyotolewa kwa Umma juu ya Mwenendo wa Kimbunga hicho imesema sababu ya kufanya kimbunga hicho kuzidi kuwa hafifu ni kutokana na kuendelea kuimarika kwa upepo kinzani katika mwelekeo wa kimbunga hicho.

Pia ilisema mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yamesambaa baharini karibu na maeneo ya kusini mwa pwani ya Tanzania na Msumbiji.

“Mwenendo wa kimbunga hafifu “Jobo” unaonesha kuwa katika kipindi cha saa sita zilizopita za Aprili 25,mwaka huu imepoteza nguvu yake wakati kiliingia nchi kavu kusini mwa mkoa wa Pwani na Dar es Salaam usiku wa Aprili 24,2021,”ilisema taarifa hiyo

Ilisema masalia ya mawingu yanayoambatana na kilichokuwa kimbunga “Jobo”yanaweza kusababisha mvua katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani.

“Tunaendelea kutoa ushauri kwa wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika,”ilisema taarifa hiyo

Ikumbukwe kuwa Aprili 21 mwaka huu,TMA ilitoa taarifa kwa umma uwepo wa Kimbunga Jobo katika bahari ya Hindi Kaskazini mwa Madagascar.

Ilisema kulijitokeza mgandamizo mdogo wa hewa ambao ulifikia kiwango cha kimbunga hafifu kwa jina la Jobo.

Kimbunga hicho kilikuwa kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar katika bahari ya Hindi umbali wa Kilometer 930 na kilometa 1030 kutoka pwani ya Lindi na Mtwara.