Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, Mbozi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ameahidi kusaidia upatikanaji wa mkopo kwa mwekezaji mwenye ulemavu, Tunginie Sanga, anayemiliki shule ya awali na msingi ya Sanga T Forest,eneo la Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe.
Akizungumza wakati wa ziara yake shuleni hapo, Februari 26, 2025,Kikwete amebainisha kuwa dhamira ya Sanga ya kuboresha sekta ya elimu ni ya kupongezwa, hivyo Serikali ina wajibu wa kumuunga mkono.

Alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi kuhakikisha mwekezaji huyo anapatiwa mkopo wa asilimia 10,unaotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Nataka ifikapo Oktoba, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, tuone maendeleo zaidi katika mradi huu baada ya kupatiwa mkopo,” amesema Kikwete.
Kwa upande wake,Tuginie Sanga,amesema tayari amewekeza milioni 79 katika ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, matundu matano ya vyoo na nyumba ya mwalimu pamoja na kuweka mkazo kwenye utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ya matunda, kivuli na maua.

Ameeleza kuwa changamoto anazokabiliana nazo na kusababisha kuomba mkopo ni ukosefu wa usafiri kwa wanafunzi,uzio wa shule, upungufu wa vyumba vya madarasa na uhaba wa vifaa vya michezo kama bembea.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alimpongeza Sanga kwa uwekezaji wake na kusisitiza kuwa elimu si biashara bali ni huduma muhimu kwa jamii huku akiahidi kushughulikia haraka usajili wa shule hiyo ili kuwezesha upatikanaji wa mkopo na kuharakisha maendeleo yake.

More Stories
Khimji kumchangia Zungu fomu ya Ubunge
Mulugo atoa rambirambi familia nne zilizopoteza wapendwa kwa ajali
Huduma kwa wateja EWURA sasa kidigitali