December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kikundi cha watu wa Kyela kuendelea kusaidia wana Kyela sekta ya afya, elimu

Na Esther Macha,Timesmajira,Online, Kyela

KIKUNDI cha Watu wa Kyela waishio maeneo mbalimbali ndani na nje ya Nchi ( IBHASA GROUP), kimewahakikishia wananchi wa Kyela kuwa wataendelea kujitoa kwa hali na mali, kusaidia  Sekta ya Afya, Elimu lengo likiwa kuboresha afya za watu hao ili waendelee kufanya shughuli za kujiletea maendeleo.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu wa IBHASA GROUP, Sady Mwang’onda amesema kwa miaka mitatu mfululizo kikundi hicho kimeendelea kuisaidia jamii ya Kyela ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kutokana na mchango mkubwa uliochangia kuwafikisha walipo sasa.

Amesema kuwa  kuelekea mwishoni mwa mwaka huu wa 2021, kundi hilo la Ibhasa linaenda kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa madawati kwa Shule kadhaa za Msingi za wilayani Kyela,kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika Wilaya hiyo ikiwemo fukwe za Ziwa nyasa na msitu wenye historia kubwa ya mambo ya kale uitwao Katago.

“Tangu mwaka  2019 Kundi la watu wa Kyela waishio ndani na nje ya nchi waliungana kwa pamoja kuchangishana michango ya fedha kwa ajili ya kuwasaidia wanakyela wenye uhitaji wa huduma za Afya  kwa kuwakatia
bima za Afya kupitia CHIF iliyoboreshwa ambapo kwa mwaka huo  kaya 100 zilifikiwa “amesema Mwang’onda .


Ameongeza  kuwa mwaka 2021  wameamua kuongeza huduma kwa wanakyela kwa kuisaidia pia sekta ya elimu ambayo bado  inauhitaji mkubwa. Aidha amesema kuwa  zaidi ya shilingi milioni mbili zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa madawati 50 kwa shule za Msingi na kwamba Ibhasa Group itakabidhi kwa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ili kuzipatia shule zenye uhitaji.

“Tumetenga kiasi cha shilingi milioni tatu kwa ajili ya  kuzisaidia Kaya 100 zenye jumla ya watu 600 zinazoishi katika mazingira magumu zitakatiwa bima ya Afya  kupitia CHIF iliyoboreshwa ili kujihakikisha matibabu kuanzia kwenye Zahanati Hospitali ya Wilaya hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,” amesema Mwang’onda.

Zaidi ya washiriki 100 wa Kundi la Ibhasa group linalohusisha watu waishio ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kurudi kwao Kyela kuisaidia jamii katika masuala ya Afya na Elimu pamoja na kufungua fursa
mbalimbali za kiuchumi kupitia ngoma za asili zilizoandaliwa,mchezo wa soka na kutembelea vivutio mbalimbali lengo likiwa ni kuijenga Wilaya ya Kyela.

Kwa upande wake katibu wa kikundi  hicho ,Nicolaus Mwangomo alisema watendelea kuisadia Jamii ya kyela katika Nyanja za kiuchumi na Kijamii ili kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa Kinara katika ufaulu wa Masomo kwa wanafunzi na wazalishaji wa mazao mbalimbali kuinua uchumi wao