Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Mtangazaji nguli, na mwandishi wa habari mashuhuri Africa Mashariki na Kati aliyekuwa akitangaza kipindi cha Dira ya Dunia katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambaye , Salim Kikeke amesema uwepo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini – TAWA katika Tamasha la Kizimkazi umekuwa chachu ya kuchagiza na kulipa hadhi tamasha hilo kutokana na Taasisi hiyo kuwapeleka wanyamapori hai ambao wamekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wengi wanaotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kikeke ameyasema hayo leo Agosti 21, 2024 alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na kufika katika bustani ya wanyamapori hai ambapo alipata fursa ya kujionea aina mbalimbali za wanyamapori wakiwemo Simba, Chui, Fisi, Chatu, Pundamilia na spishi za aina tofauti za ndege nyuni.
“Niko hapa Kizimkazi kwa ajili ya Tamasha la Kizimkazi na nimefurahi sana kutembelea banda hili la TAWA…kuna mabanda mengi sana lakini TAWA wameweza kuleta kivutio cha kipekee kabisa, wameleta wanyama mbalimbali na zaidi ni kuonesha hazina ya Taifa letu” amesema
“Nadhani kitu TAWA wanakifanya ni muhimu sana kuweza kuja kutoa elimu na kufahamisha jamii yetu ya hapa hapa nyumbani lakini vilevile watu wanaotoka nje ya Taifa letu kufahamu maana halisi ya wanyama hawa, jinsi tunavyowatunza na jinsi wanavyolisaidia Taifa letu kwa njia ya kipato kwahiyo pongezi nyingi sana kwa TAWA kwa kile wanachokifanya uwepo wao nadhani umeongeza ile hadhi ya Kizimkazi” ameongeza na kusisitiza Kikeke
TAWA ni mojawapo ya Taasisi za Serikali zinazoshiriki katika Tamasha hilo kwa lengo la kutangaza fursa za utalii zilizopo katika maeneo yake ya kimkakati yaliyo chini ya usimamizi wake hususani ya ukanda wa Kusini Mashariki Kama vile Hifadhi za Selous, Kilwa, Pande (Dar es Salaam), Wamimbiki (Pwani/Morogoro), ikiwa ni muendelezo wa kuunga mkono jitahada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotangaza vivutio vya Utalii wa nchi yetu kupitia filamu Maarufu za Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais