November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Masumbuko Lamwai

Kifo cha Dkt.Lamwai chatikisa kila kona

Na Mwandishi Wetu

KIFO cha mwanasheria nguli na wakili wa kujitegemea, Dkt. Masumbuko Lamwai, kimepokewa kwa mshtuko na Watanzania wengi kutokana na umaarufu aliojijengea katika fani hiyo na kwenye siasa za Tanzania.

Kifo cha Dkt. Lamwai kilitokea jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana na kuthibitishwa na mdogo wake ambaye ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini.

Baadhi ya wasomaji wa gazeti hili waliozungumza jana kwa nyakati tofauti, walisema kifo cha Dkt. Lamwai sio pigo kwa familia yake pekee tu, bali hata kwa tasnia ya sheria na siasa kwa ujumla.

“Mungu alimpa kipaji cha kujenga hoja awe mahakamani au hata kwenye siasa. Wanasheria wengi hapa nchini wamepikwa na Dkt. Lamwai wakati akifundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na vyuo vingine kikiwemo cha Tumaini,” alisema mmoja wa wanasheria, Lameck Paul na kuongeza;

“Pengo lake hajaliacha kwenye familia peke yake, kwani hata tasnia ya sheria imepoteza mtu muhimu.”

Mara baada ya taarifa za kifo cha Dkt. Lamwai kuanza kusambaa baadhiya wasomaji wa gazeti hili walipiga simu ili kupata uthibitisho wa taarifa hizo.

Mdogo wake Dkt. Lamwai ambaye ni Mbunge wa Rombo kwa tiketi ya CHADEMA, Selasini, alisema kaka yake alikuwa mwanasheria na mhadhiri na afya yake ilidhoofika wiki mbili zilizopita na baadaye alishikwa na malaria kabla ya umauti kumfika.

Akizungumza jana Selasini alisema licha ya kusumbuliwa na malaria, Dkt. Lamwai alikuwa akiendelea kupata dawa hadi hali yake ilipobadilika tena jana usiku (juzi) na kukimbizwa hospitali.

“Afya yake ilidhoofu katika kipindi cha wiki mbili zilizopita lakini pia alipigwa na malaria kali ambayo alikuwa anaendelea kupata dawa, hata Jumapili alikaa na watoto wake wakaongea ongea sana ni kwa vile tu mtu huwezi kujua Mungu amepanga uondoke saa ngapi, jana usiku (juzi) ndiyo akazidiwa na akafariki njiani wakati anapelekwa hospitali, mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo,” alisema Selasini.

Mbunge Selasini ameongeza kuwa kaka yao huyo alikuwa ndiye kiongozi wa familia na hata baada ya wazazi wao kufariki, yeye alibaki kuwa nguzo kwa kuwaongoza kwa hekima na busara.

Aidha alisema Dkt Lamwai, licha ya kuwa Mwanasheria pia aliwahi kuwa diwani wa Manzese na hatimaye kuwa Mbunge wa Ubungo. Aliwahi pia kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa na Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam.

Umaarufu wa Dkt. Lamwai

Dkt. Lamwai alipata umaarufu kisiasa mwaka 1995 baada kugombea ubunge katika Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi na kufanikiwa kumshinda aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Venance Ngulla.

Alikuwa ni miongoni mwa wabunge wa kwanza kuingia bungeni baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Baada ya kuingia bungeni akiwa na wabunge wengine wa upinzani kutoka NCCR-Mageuzi akiwemo Mabere Marando, James Mbatia na wengine walileta msisimko mkubwa bungeni.

Spika wa Bunge wakati huo, Pius Msekwa alikumbana na changamoto ya kuongoza Bunge hilo ambalo lilikuwa na wabunge machachari, wakiwemo wanasheria nguli Dkt. Lamwai na Marando, ambapo walijenga hoja iliyosababisha kiapo walichokuwa wakiapa wabunge kubadilishwa na kuapishwa upya.

Lakini pia wakati matokeo ya urais yakiendelea kutangazwa mwaka 1995, ambapo mchuano mkali ulikuwa baina ya mgombea wa NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema dhidi ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa, Dkt. Lamwai aliongoza jopo la wanasheria wa chama hicho kwenda kupinga matokeo hayo kutangazwa mahakama kuu kutokana na sababu mbalimbali, lakini maombi yao yalikataliwa na mahakama.

Katika kinyang’anyiro hicho, Mkapa aliibuka mshindi na kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa Rais wa Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baadaye Dkt. Lamwai alihama upinzani na kujiunga na CCM ambapo aliteuliwa na Rais Mkapa (wakati huo Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne) kuwa mbunge wa kuteuliwa na rais.

Baada ya kumaliza muda wake wa ubunge Dkt. Lamwai alijikita kwenye taaluma yake ya uanasheria na mhadhiri akifundisha vyuo vikuu.