January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiduku ataka rekodi mpya kwa Sirimongkhon Lamthuam.

Na Angela Mazula,TimesMajira Online.

BONDIA wa kimataifa wa Tanzania ambaye ameshawahi kushinda ubingwa wa IBF, UBO na Ubingwa wa Taifa, Twaha Kassim ‘Kiduku’ametamba kuweka rekodi mpya katika pambano lake la kuwania ubingwa wa Dunia wa WBC dhidi ya Sirimongkhon Lamthuam kutoka nchini Thailand katika pambano la raundi 12 la uzani wa Super Welter litakalofanyika Oktoba 30 katika ukumbi wa PTA.

Kiduku atapambana na bondia huyo anayeshika nafasi ya kwanza nchini Thailand na 205 kati mabondia 1202 duniani kwenye uzani wa Light Heavy, ambaye amekubali kushusha uzani ili kupigana katika pambano hilo.

Mpinzani wa Kiduku pia anatamba kwa rekodi nzuri aliyoiweka kwani katika mapambano 101 aliyocheza ameshinda mapambano 97, 62 kwa KO na kupoteza mapambano manne wakati yeye akicheza mapambano 22 ambayo ameshinda 17, tisa kwa KO amepoteza mapambano sita na kutoa sare katika pambano moja.

Akizungumzia maandalizi yake kuelekea kwenye pambano hilo, Kiduku amesema kuwa, licha ya rekodi zake kuzidiwa mara dufu na mpinzani wake lakini hatojali kwani anachokitaka ni kuweka heshima mpya katika pambano hilo ambalo linamfanya kuwa bondia wa kwanza kutoka nchini kuwania ubingwa huo.

Kwake kucheza pambano ya kuwania mkanda wa WCB unaotambulika Dunia nzima ni heshima kubwa na ubora wa bondia mpinzani wake utawafanya makocha wake kumzidishia dozi ya mazoezi ili kuhakikisha anafanya vizuri.

“Bondia ambaye nimechaguliwa kupigana naye ni tofauti sana na waliopambana na mabondia wenzangu kwani hata rekodi zake zinajieleza, lakini ninachopenda kuwaahidi ni kuwa ubora wake ndio utakaonipa kasi na maandalizi ya tofauti kabisa kwani makocha wangu Power Ilanda na Simon Ponera wananisimamia vizuri katika maandaliz,”.

“Lakini pia kila siku nazidi kumuomba Mungu anijaalie afya iliyo njema ili kufanya mambo mazuri katika siku ya pambano langu na kuendelea kuipeperusha vema bendera ya nchi yangu ,” amesema Kiduku.

Licha ya kuzungumzia pambano hilo lakini bondia huyo pia ameweka wazi kuwa sababu zilizomfanya kutaka mapamabano dhidi ya Dulla Mbabe na Hassan Mwakinyo ni kutaka kupanda katika rekodi za ngumi na si kuweka wazi nani zaidi kama wanavyotaka watanzania wengi.

Amesema, katika rekodi Dulla Mbabe anashika nafasi ya 70 na kumsinda Mwakinyo kwani nilichokuwa nataka ni kufaidika kwani yeyote ambaye angeshinda pambano hilo basi rekodi zitambeba.

“Ukiangalia mimi nina nyota mbili na nusu sawa na Dulla Mbabe na Mwakinyo hivyo yeyote atakayempiga mwenzake atanufaika na sikuwataka kudhihirisha nani zaidi lakini ikitokea Mwakinyo leo akakubali kupigana na mimi na kunipiga atakuwa amenufaika katika rekodi,” amesema Kiduku.

Baada ya pambano hilo dhidi ya Mthailand ambalo anatarajia kushinda hana shaka atapanda mara dufu kwenye viwango vya dunia na kipindi hicho Mwakinyo ambaye amekuwa akimkwepa mara kadhaa ndiye ataomba kupigana naye.

Akizungumzia pambano hilo, Mkurugenzi wa kampuni ya Golden Boy Afrika ambao ndio waratibu wa pambano hilo, Shomari Kimbau amesema kuwa, watahakikisha pambano hilo linakuwa la aina yake kwani ndio mara ya kwanza pambano la kuwania mkanda wa WBC kuja kucheza katika nchi za Afrika na zaidi katika nchi ya Tanzania .

Amesema kuwa, sababu hiyo pekee ndiyo itakayofanya mchezo huo kuwa wa kipekee kwa sababu mashabiki wote duniani watakuwa na uwezo wa kuangalia pambano hilo ambalo litafanyika katika viwanja vya TPA.

Pambano hilo la ubingwa wa WBC litatanguliwa na mapambano mengine ya utangulizi yatakayowakutanisha Alphone Mchumiatumbo dhidi ya Jongo Jongo huku bondia Maono Ally atapanda ulingoni kuzichapa na Joseph Sinkala.

Mapambano mengine yatawakutanisha Saidi Juma atacheza na Ibrahim Tamba, Hamza Iddy atapambana na Jamal Kunoga wakati Ruth Chisale akioneshana ubabe na Sijali Saidi.

Hata hivyo Kimbau amesema kuwa, wana uhakika Kiduku atashinda pambano hilo na kuingia katika levo nyingine na wapo tayari kumfata tena Mwakinyo wakimuwekea mezani dau la dola 2000 mara mbili ya lile alilolitaka awali ili kupambana na Kiduku.